9.3 C
New York

Estevao, Yamal na vita ya ufalme

Published:

LONDON, Uingereza
WAKATI Chelsea ikiitandika Barcelona mabao 3-0 katika mchezo wa usiku wa jana wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Estevao alikuwa mwiba mchungu kwa Wacatalunya hao.
Si tu alifunga bao la pili katika dakika ya 55, pia aliipa wakati ngumu safu ya ulinzi ya Barcelona kwa kasi yake, uwezo wa kumiliki mpira na ubunifu mkubwa alionao miguuni.
Kabla ya timu hizo kukutana katika Uwanja wa Stamford Bridge, kinda mwenzake, Lamine Yamal, ndiye aliyekuwa akitabiriwa kuteka ‘shoo’, jambo ambalo hata hivyo halikutokea.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Yamal na Estevao kukutana baada ya miezi mingi ya makinda hao kutajwa kuwa ni miongoni mwa vipaji vikubwa vya soka vilivyopo Ulaya Kwa sasa.
Nyota hao walizaliwa mwaka 2007 na sasa kila mmoja ana umri wa miaka 18, licha ya kwamba tayari majina yao ni makubwa katika ulimwengu wa soka.
Kwa mujibu wa mtandao wa CIES Football Observatory, Estevao na Yamal ndiyo makinda wenye thamani kubwa zaidi kwa sasa kwenye soko la usajili.
Hata hivyo, Yamal raia wa Hispania anaongoza akiwa na thamani ya Pauni milioni 307.4, wakati Estevao wa Brazil ana Pauni milioni 103.8.
Yamal, kwa upande mwingine, alishika nafasi ya pili msimu huu wa tuzo ya Ballon d’Or iliyotua kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Ousmane Dembele.
Alishika nafasi ya pili kutokana na mafanikio yake ya msimu uliopita, ambapo nyota huyo aliiongoza Hispania kutwaa taji la EURO akiwa na umri wa miaka 17.
Wakati huo huo, kama itakumbukwa, Yamal ametwaa mara mbili tuzo ya Kopa, ambayo hupewa Kinda Bora wa Mwaka.
Kwa sasa, ameshafikisha mabao 31 na ‘asisti’ 42 katika mechi 119, pia akiwa ameingia kambani sita kwa michezo 23 aliyoitumikia Hispania. Ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia nchi yake.
Estevao, kwa upande wake, ameshazifumania nyavu mara tano na kutoa asisti moja katika michezo yake 11 ndani ya kikosi cha Chelsea.
Kabla ya kusajiliwa na Blues, aliifungia mabao 27 na asisti 15 katika mechi 83 alipokuwa akiitumikia Palmeiras ya Ligi Kuu nchini Brazil.
Akiwa na timu yake ya taifa ya Brazil, kinda huyo amefunga mabao matano katika mechi 11 alizocheza.
Kutokana na viwango bora vya wachezaji hao, baadhi ya mashabiki wameanza kuufananisha upinzani wao na ule wa malejendari wa soka, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
Lakini, kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, anaona bado ni mapema mno kwa Estevao na Yamal kuwekewa daraja moja na wakongwe hao.
“Ni mapema sana kwao kufananishwa na Messi na Ronaldo. Estevao na Lamine bado ni makinda, kuwafananisha na Messi na Ronaldo ni kuwaongezea presha.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img