12.7 C
New York

Makocha wazawa Afrika watakaotamba Kombe la Dunia 2026

Published:

CAIRO, Misri
KWA mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, fainali za mwakani zitazihuhudia timu nyingi za Afrika zikiwa chini ya makocha wazawa.
Kati ya mataifa tisa yatakayoiwakilisha Afrika kwenye michuano hiyo, saba yamekabidhi majukumu ya kuzinoa timu zao kwa makocha wazawa.
Otto Addo (Ghana)
Nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana ‘Black Stars’ alianza safari yake ya ukocha akiwa Borussia Dortmund. Mwaka 2021, aliajiriwa kuwa msaidizi wa aliyekuwa kocha wa Black Stars, Milovan Rajevac.
Addo aliajiriwa rasmi kuwa kocha mkuu mwaka 2022, ambapo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa zamani wa Black Stars kuinoa timu hiyo katika fainali za Kombe la Dunia.
Baada ya kumalizika kwa fainali hizo, Addo alirejea kuzinoa timu za vijana za Dortmund, kabla ya Ghana kumrudisha Machi, mwaka jana.
Oktoba, mwaka huu, aliiongoza Ghana kufuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Comoro. Anakuwa kocha wa kwanza mzawa kuiongoza Ghana kwa misimu miwili mfululizo ya Kombe la Dunia.
Walid Regragui (Morocco)
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Morocco na sasa ndiye mkuu wa benchi la ufundi tangu alipokabidhiwa mikoba hiyo Agosti, 2022.
Licha ya kuajiriwa miezi michache kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia, Regragui aliushangaza ulimwengu. Morocco iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika nusu fainali ya michuano hiyo.
Ni kutokana na mafanikio hayo, alitangazwa kuwa Kocha Bora wa Mwaka 2023 wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Akiwa pia na rekodi ya kutwaa mataji akiwa na klabu za FUS Rabat na Wydad Casablanca, Regragui ameiongoza Morocco kucheza mechi 17 bila kufungwa, ameshinda 16 na sare moja.
Pape Thiaw (Senegal)
Mshambuliaji wa kati wa zamani wa timu ya taifa ya Senegal. Thiaw alianza kuheshimika katika taaluma ya ukocha mwaka 2022, baada ya kutwaa taji la fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Desemba, mwaka jana, ndipo alipopandishwa na kukabidhiwa timu ya wakubwa, akichukua nafasi ya mkongwe mwenzake, Aliou Cisse.
Awali, alikuwa kocha wa muda lakini aliaminiwa moja kwa moja baada ya kuiongoza Senegal kushinda mechi nne mfululizo bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Emerse Fae (Ivory Coast)
Kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Ivory Coast. Aliajiriwa kama kocha wa muda mwaka jana baada ya Jean-Louis Gasset kufungashiwa virago wakati fainali za AFCON zikiendelea.
Licha ya presha kubwa, Fae aliiongoza Ivory Coast kutwaa ubingwa wa fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa kuzing’oa Senegal, Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Katika mchezo wa fainali, walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nigeria na hilo likawa taji la tatu la AFCON kutua Ivory Coast.
Fae anakuwa kocha wa kwanza raia wa Ivory Coast kuiongoza timu hiyo katika fainali za Kombe la Dunia.
Bubista (Cape Verde)
Jina kamili ni Pedro Leitao Brito na ni beki wa zamani wa timu ya taifa ya Cape Verde. Bubista alianza kukinoa kikosi hicho Januari, 2020.
Akiwa kocha wa Madagascar ‘Blues Sharks’, aliiongoza timu hiyo kufuzu fainali za AFCON za mwaka 2021, kisha akaifikisha robo fainali ya michuano hiyo msimu uliofuata (2023).
Safari hii, ameiwezesha Cape Verde kufuzu kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia, hiyo ikimpa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka huu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Hossam Hassan (Misri)
Mpachikaji mabao wa zamani wa timu ya taifa ya Misri. Hassan aliajiriwa kuliongoza benchi la ufundi la kikosi hicho Februari, mwaka huu.
Kabla ya kupewa mikoba hiyo, aliwahi kufanya kazi katika ngazi ya klabu, ambapo kwa nyakati tofauti alizinoa Zamalek, Al-Masry, Ismaily na Pyramids.
Hassan anasifika zaidi kwa soka la kujilinda, pia ni muunini wa kushambulia kwa kutumia viungo wa pembeni.
Sami Trabelsi (Tunisia)
Beki wa kati wa zamani wa timu ya taifa ya Tunisia. Hii ni mara yake ya pili kukinoa kikosi hicho baada ya ajira ya kwanza mwaka 2011 hadi 2013.
Akiwa kwenye benchi mwaka 2011, itakumbukwa kuwa Trabelsi aliiwezesha Tunisia kutwaa ubingwa wa fainali za CHAN.
Baada ya miaka zaidi ya 10 ya kufanya kazi nje ya nchi, ikiwamo kuinoa Al-Sailiya ya Qatar, alirejea kuinoa Tunisia mwanzoni mwa mwaka huu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img