MONTEVIDEO, Uruguay
KUELEKEA fainali za Kombe la Dunia za mwakani, Uruguay inashika nafasi ya 16 katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
‘La Celeste’ ni mabingwa mara mbili wa fainali za Kombe la Dunia. Walitwaa ubingwa wa michuano hiyo katika miaka ya 1930 na 1950.
Katika fainali zijazo zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico, itakuwa ni mara ya 15 kwao kushiriki Kombe la Dunia.
Wakati huo huo, Uruguay ni mabingwa mara 15 wa Copa America, wakifanya hivyo katika miaka ya 1916, 1917, 1920, 1923, 1924, 1926, 1935, 1942, 1956, 1959, 1967, 1983, 1987, 1995 na 2011.
Msimu uliopita wa Kombe la Dunia, 2022, waliishia hatua ya makundi na sasa wanajitafuta wakiwa bila Luis Suarez na Edinson Cavani waliostaafu kuitumikia timu ya taifa mwaka jana.
Hata hivyo, kikosi chao kina wachezaji wazuri kwa sasa. Miongoni mwao ni staa wa zamani wa Liverpool anayekipiga Al Hilal ya Saudi Arabia, Darwin Nunez. Alifunga matano katika mechi za kufuzu.
Pia, wapo nyota wengine wanaofanya vizuri katika ulimwengu wa soka, wakiwamo Federico Valverde (Real Madrid) na Giorgian de Arrascaeta (Flamengo).
Kwa upande mwingine, Uruguay wanajivunia uzoefu wa kocha mkongwe raia wa Argentina, Marcelo Bielsa, aliyeajiriwa mwaka 2023.
Bielsa mwenye umri wa miaka 70, hii ni mara yake ya tatu kushiriki Kombe la Dunia akiwa na kwenye benchi la ufundi na timu tofauti.
Mwaka 2002, kocha huyo wa zamani wa Leeds United aliiongoza Argentina, ambayo hata hivyo iliishia makundi. Mwaka 2010, aliiongoza Chile kufika hatua ya 16 Bora.
Published:


