MUNICH, Ujerumani
IKIWA nafasi ya tisa katika viwango vya ubora wa soka duniani, Ujerumani ni sehemu ya mataifa 48 yatakayoshiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia.
Timu yake ya taifa ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia. Walitwaa ubingwa huo katika miaka ya 1954, 1974, 1990 na 2014.
Wakati huo huo, Ujerumani ni mabingwa mara tatu wa fainali za Mataifa ya Ulaya (EURO), ambapo walibeba taji hilo katika miaka ya 1972, 1980 na 1996.
Watashiriki fainali zijazo wakiwa chini ya kocha Julian Nagelsmann. Amekuwa na kikosi hicho tangu alipoajiriwa Septemba, 2023.
Nagelsmann aliyewahi pia kuinoa Bayern Munich, alichukua nafasi ya Hansi Flick ambaye alifukuzwa akiwa ameiongoza Ujerumani katika mechi 25 tu.
Katika kile kilichoonekana kuwa ni mwanzo mzuri kwa Nagelsmann, Ujerumani ilifika robo fainali katika fainali za EURO za mwaka jana.
Nyota wakubwa wanaounda kikosi kwa sasa ni Florian Wirtz (Liverpool), Serge Gnabry (Bayern Munich) na Nick Woltemade (Newcastle).
Katika mechi za kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia, Woltemade aliifungia timu hiyo jumla ya mabao manne.
Tangu walipotwaa ubingwa mwaka 2014, fainali za Kombe la Dunia hazijawa nzuri kwa Ujerumani. Hawajawahi kuvuka makundi tangu kipindi hicho.
Swali ni je, nini ambacho Ujerumani itakifanya katika msimu wake wa 21 wa fainali za Kombe la Dunia?
Published:


