SEOUL, Korea ya Kusini
KWA sasa, Korea Kusini inashika nafasi ya 22 katika viwango vya ubora wa soka duniani. Iliwahi kupanda hadi nafasi ya 17 na hiyo ilikuwa mwaka 1998.
‘Taegeuk Warriors’ ni mabingwa mara mbili wa Kombe la Asia, wakifanya hivyo katika miaka ya 1956 na 1960 na hii ni mara yao ya 12 kushiriki Kombe la Dunia.
Mafanikio yao makubwa zaidi katika mashindano hayo ni kufika nusu fainali wakiwa wenyeji mwaka 2002.
Mchezaji tegemeo zaidi kwao katika fainali zijazo ni nahodha wa kikosi, Heung-Min Son, ambaye alifunga mabao 10 katika mechi za kufuzu.
Son aliyewahi kukipiga Tottenham na sasa yuko Los Angeles ya Marekani, ameweka wazi kuwa fainali zijazo zitakuwa za mwisho kwake, kabla ya kustaafu kuitumikia timu ya taifa.
Aidha, katika kikosi chao pia wapo wachezaji walio kwenye ubora mkubwa, wakiwamo Hwang Hee-Chan (Wolves) na Lee Kang-In (PSG).
Kocha wa kikosi hicho kwa sasa ni Hong Myung-Bo, ambaye aliajiriwa Julai, mwaka jana, na hii ni mara yake ya pili kuinoa Korea ya Kusini.
Myung-Bo aliyeshiriki mara nne Kombe la Dunia akiwa mchezaji, ikiwamo mwaka 2002 alipokuwa nahodha, alikuwa kocha wa timu hiyo katika fainali za mwaka 2014.
Kama itakumbukwa, alijiuzulu baada ya Korea ya Kusini kuondoshwa kwenye michuano hiyo ikiwa haijashinda hata mechi moja.
Published:


