LONDON, Uingereza
TIMU ya taifa ya England ‘Three Lions’ ni mabingwa wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1966. Wanashika nafasi ya nne kwa ubora duniani.
Kama itakumbukwa, England ilikuwa timu ya kwanza barani Ulaya kufuzu fainali za mwakani. Ni mara yao ya nane mfululizo tangu waliposhindwa kufuzu mwaka 1994.
England walikata tiketi yao kwa ushindi wa mechi zote za kufuzu, tena bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa. Ni kwa mara ya kwanza barani Ulaya tangu Yugoslavia ilipofanya hivyo mwaka 1954.
Kocha ni Thomas Tuchel aliyeajiriwa Januari, mwaka huu. Tuchel anakuwa kocha wa kwanza raia wa Ujerumani kuliongoza benchi la ufundi la Three Lions.
Kikosi chake kina mastaa wengi, wakiwamo Harry Kane (Bayern Munich), Jude Bellingham (Real Madrid) na Bukayo Saka (Arsenal).
Kane ndiye aliyekuwa na mchango mkubwa zaidi katika mechi za kufuzu, ambapo straika huyo aliifungia timu yake jumla ya mabao nane.
Kwa siku za hivi karibuni, kocha Tuchel amekuwa akilaumiwa kwa kitendo chake cha kutowajumuhisha kikosini mastaa Jude Bellingham na Phil Foden.
Katika hatua nyingine, England wanakwenda Kombe la Dunia kwa mara yao ya 17, safari hii wakiwa wametoka kufika hatua ya fainali ya EURO kwa misimu miwili mfululizo.
Published:


