ZAGREB, Croatia
NAFASI ya 10 kwenye viwango vya ubora wa soka duniani. Croatia wamepromoka kwa nafasi saba, tofauti na nafasi ya tatu waliyokuwa mwaka 1998.
Licha ya kuwa ni Taifa lenye watu milioni nne pekee, Croatia imekuwa ikitoa ushindani mkubwa kwa vigogo wa soka barani Ulaya.
Hata hivyo, ‘Kockasti’ haijawahi kuwa mabingwa wa michuano yoyote mikubwa, licha ya kuzalisha vipaji vingi katika ulimwengu wa mchezo wa kandanda.
Ni miongoni mwa mataifa yaliyodumu na kocha mmoja kwa muda mrefu. Zlatko Dalic aliyeajiriwa mwaka 2017.
Dalic ni mmoja kati ya makocha wenye heshima kubwa katika soka la kimataifa. Ndiye aliyeifikisha fainali (Kombe la Dunia) mwaka 2018, pia akiiwezesha kushika nafasi ya tatu mwaka 2022.
Katika mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwakani, Andrej Kramaric alikuwa shujaa wao baada ya kufunga mabao sita.
Nyota wengine wanaokipa jeuri ya kufanya vizuri msimu ujao wa michuano hiyo ni Luka Modric (AC Milan), Ivan Perisic (PSV) na Josko Gvardiol (Manchester City).
Msimu ujao unaweza kuwa wa mwisho kwa Modric, wakati Perisic na Kramaric nao wakionekana kubakiza miaka michache tu kabla ya kustaafu.
Baada ya kuishia makundi mara tatu mfululizo, Croatia walifika fainali mwaka 2018, kabla ya kushika nafasi ya tatu misimu uliopita (2022) nchini Qatar.
Wakati huo huo, chini ya kocha Dalic, timu hiyo ilifika fainali katika michuano ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya (Nations League) mwaka 2023.
Hii inakuwa mara ya saba kwa Croatia kushiriki fainali za Kombe la Dunia. Je, kuna maajabu ya kusubiri hapo mwakani?
Published:


