VIENNA, Austria
MWAKA 2016, Austria ilipanda hadi nafasi ya 10 katika viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Kwa sasa, iko nafasi ya 24.
Ikiwa haijawahi kutwaa taji kubwa, kwa sasa timu yake ya taifa inanolewa na kocha mzawa, Ralf Rangnick, ambaye aliajiriwa mwaka 2022.
Rangnick aliamua kubaki kwenye benchi la Austria, licha ya kuwekewa ofa nono na Bayern Munich mwaka jana. Ameiwezesha Austria kurudi Kombe la Dunia baada ya miaka 28 ya kuzikosa fainali hizo.
Kikosi cha kocha huyo wa zamani wa Manchester United kina wachezaji kadhaa wanaowika Ulaya, wakiwamo Marko Arnautovic (Red Star), David Alaba (Real Madrid) na Marcel Sabitzer (Borussia Dortmund).
Austria iliyofika hatua ya 16 Bora katika michuano ya EURO 2020 na 2024, inakwenda Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu iliposhiriki fainali hizo mwaka 1998.
Katika mara zao tano za ushiriki wa Kombe la Dunia hivi karibuni, Austria haijawahi kuvuka hatua ya makundi.
Mara yao ya mwisho, 1998, walishindwa kuingia hatua ya 16 Bora katika kundi lililokuwa na Italia, Chile na Cameroon.
Published:


