10.9 C
New York

Soma hapa maajabu ya Haiti kufuzu Kombe la Dunia

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
TIMU ya taifa ya Haiti nayo imefanikiwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwakani katika mazingira yaliyowashangaza wengi.
Haiti, ambao hii ni mara yao ya pili kushiriki, walijihakikishia nafasi baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Nicaragua.
Hata hivyo, safari hii walifuzu kwa staili ya aina yake, ambapo ukweli ni kwamba kocha wao, Sebastien Migne, hajawahi kufika katika Kisiwa hicho tangu aajiriwe.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 52 aliajiriwa miezi 18 iliyopita lakini hajaweza kuingia Haiti kutokana na hali mbaya ya usalama nchini humo.
Amekuwa akikutana na wachezaji wake katika Kisiwa cha Curacao, ambacho kipo umbali wa maili 500 kutoka Haiti.
Tangu Haiti ilipokumbwa na tetemeko kubwa la ardhi mwaka 2010, nchi hiyo imekuwa kwenye hali mbaya ya usalama kutokana na magenge ya uhalifu kujimilikisha maeneo, hasa ya Mji Mkuu wa Port-au-Prince.
Ni kutokana na migogoro mingi katika taifa hilo, watu milioni 1.3 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, huku balaa la njaa likiwepo kwa kiasi kikubwa.
Watalii hawafiki tena katika Kisiwa hicho chenye watu milioni 12 wakihofia matukio ya utekaji na uhalifu mwingine.
“Ni ngumu (kucheza soka Haiti) kwa sababu hali ni ya hatari mno,” alisema kocha Migne akihojiwa na jarida la France Football.
“Mara zote nimekuwa nikiishi katika nchi ninazoajiriwa lakini siyo kwa hapa. Hakuna tena ndege za kimataifa zinazotua pale.”
Migne, ambaye alikuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Cameroon katika fainali za Kombe la Dunia zilizopita, amekuwa akiwafuatilia wachezaji wa ndani ya Haiti kwa njia ya simu.
Akiwa nje, amekuwa akizungumza kwa simu na viongozi wa Shirikisho la Soka la Haiti, ambao humpa taarifa juu ya wachezaji wa ndani wanaofanya vizuri.
Kwa sasa, wachezaji wote waliopo kikosini ni wale wanaoishi nje ya Haiti, akiwamo kiungo wa Wolves, Jean-Ricner Bellegarde.
Pia, zipo jitihada za Shirikisho la Soka la Haiti kumshawishi mshambuliaji wa Sunderland, Wilson Isidor, aitumikie Haiti, ambako ndiko walikozaliwa wazazi wake.
Migne, kama itakumbukwa, aliwahi kuwa kocha wa timu ya soka ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ kuanzia Mei, 2018, hadi Agosti, 2019.
Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilimfuta kazi, licha ya kwamba Migne aliipeleka timu hiyo kwenye fainali za AFCON baada ya mashabiki kusubiri kwa miaka 15.
Sasa, baada ya kufuzu fainali zijazo, hii inakuwa mara ya pili kwa Haiti kucheza Kombe la Dunia, wakiwa na kumbukumbu ya kucheza mwaka 1974.
Waliposhiriki kwa mara ya kwanza, waliishia hatua ya makundi baada ya kufungwa mechi zote tatu dhidi ya Italia, Poland na Argentina.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img