15.2 C
New York

Pochettino bado hali tete Marekani

Published:

LOS ANGELES, Marekani
BAADA ya timu ya soka ya taifa ya Marekani kuishia hatua ya makundi katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022, alitafutwa kocha ambaye angeipaisha zaidi.
Shirikisho la Soka la Marekani (USSF) lilihitaji kocha ambaye angeisaidia timu hiyo kufanya vizuri zaidi katika fainali za mwaka 2026 zitakazofanyika nchini humo.
USSF ilimpa ajira Mauricio Pochettino ikiamini katika uzoefu wake wa kuzinoa Tottenham, PSG na Chelsea na kufanya kazi na wachezaji wenye majina makubwa, wakiwamo Lionel Messi, Kylian Mbappe na Neymar.
Hata hivyo, tangu raia huyo wa kimataifa wa Argentina alipoanza kuinoa Marekani, hajaonekana kupata mafanikio. Ni kama bado Marekani inahitaji kocha wa kuipa mafanikio.
Licha ya kutokupoteza katika mechi nne mfululizo za hivi karibuni, Pochettino amekuwa akikosolewa kwa mambo makubwa mawili.
Mosi, Marekani haina kikosi cha kwanza cha uhakika. Kwa nyakati tofauti, kikosi chake kimehusisha wachezaji 71.
Pili, ni kitendo chake cha kutowatumia baadhi ya wachezaji wanaoweza kuisadia timu. Katika hali ya kushangaza, amekuwa hamtumii staa wa Juventus, Weston McKennie.
Si tu kuwaacha wachezaji walio kwenye kiwango bora, amekuwa akiwaita wasiopata nafasi kubwa ya kucheza katika klabu zao.
Mathalan, licha ya kusisitiza kuwa angeita wachezaji wanaopata nafasi katika klabu zao, Pochettino alimwita staa wa Borussia M’gladbach, Gio Reyna, akiwa amecheza mechi sita pekee za Bundesliga.
Reyna ambaye msimu uliopita alicheza mechi 26 pekee, pia akiwa ameitumimia timu ya taifa mara moja tangu zilipomalizika fainali za Copa America za mwaka jana.
Alipomwita Reyna, Pochettino alikuwa amewaacha mastaa kama Antonee ‘Jedi’ Robinson, Yunus Musah, Tyler Adams, Chris Richards na Christian Pulisic, ingawa wapo waliokuwa na sababu za msingi, ikiwamo majeraha.
Sasa, wakati ukosolewaji ukiendelea, zimekuwapo tetesi za Pochettino kuondoka katika benchi la ufundi la Marekani, akihusishwa na mpango wa kurejea Ligi Kuu ya England (EPL).
Kwa upande wa EPL, klabu zinazotajwa kumtaka kocha huyo ni Manchester United, Brentford na Tottenham aliyowahi kufikisha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tottenham ilipomfuta kazi Ange Postecoglou ilitajwa kuwasiliana na Pochettino, ambaye pia hivi karibuni alikiri kutamani kufanya kazi tena Ligi Kuu ya England. “… Ninafurahia hapa Marekani lakini natamani siku moja kurudi Ligi Kuu (ya England),” alisema.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img