18 C
New York

DRC na safari ya jasho, damu kuwania tiketi Kombe la Dunia 2026

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
TIMU ya soka ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itaiwakilisha Afrika katika mchujo wa mwisho wa kupata timu moja ya kwenda fainali za Kombe la Dunia za mwakani.
DRC ilipata nafasi hiyo baada ya ushindi wa penalti dhidi ya Nigeria katika mchezo wa ‘playoff’ uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 mjini Rabat, Morocco.
Hivyo, DRC itacheza playoff nyingine Machi, mwaka huu, itakayoshirikisha mataifa kutoka mabara manne, yakigombea nafasi moja tu ya kwenda kwenye michuano hiyo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Safari yao ya kibabe
Ikiwa haijashiriki Kombe la Dunia tangu mwaka 1974, DRC ilikutana na Super Eagles baada ya kuing’oa Cameroon katika mchezo wa kwanza wa playoff.
Kabla ya kufika hapo, DRC ilionesha kiwango kizuri katika hatua ya makundi, ambapo ilikuwa Kundi B na kumaliza ikiwa nafasi ya pili, nyuma ya Senegal kwa tofauti ya pointi mbili tu.
DRC wangeweza kufuzu moja kwa moja endapo wangeifunga Senegal katika mchezo wa Septemba 9, mwaka huu, lakini waliangukia pua kwa kichapo cha mabao 3-2.
Katika hatua ya kufuzu, DRC imefunga mabao 15 na ni miongoni mwa timu sita pekee zilizoruhusu mabao machache (6), pia ikiwa na mechi sita bila nyavu zake kutikiswa.
Mwamba huyu hapa
DRC inapata mafanikio makubwa chini ya kocha raia wa Ufaransa, Sebastien Desabre, ambaye alichukua nafasi ya Hector Cuper mwaka 2022 baada ya timu hiyo kushindwa kufuzu fainali zilizopita za Kombe la Dunia.
Alipofika, Desabre aliweka wazi kuwa mpango wake ni kuhakikisha DRC inakuwa moja kati ya timu tishio ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025.
Kwa miaka mitatu sasa, kocha huyo amekuwa akishirikiana kwa karibu na Shirikisho la Soka la DRC, ikiwamo kuanzisha na kusimamia programu za soka la vijana.
Matokeo yake ni kwamba nusu ya wachezaji walioanza katika kikosi kilichoifunga Nigeria ni wale aliowaibua, ambao hawakuwahi kuwa sehemu ya timu ya taifa ya DRC.
Tuhuma za ushirikina
Ziliibuliwa na kocha wa Nigeria, Eric Chelle. Kwa mujibu wa raia huyo wa Ivory Coast, wachezaji wa DRC walifanya vitendo vya kishirikina wakati timu hiyo zilipokuwa kwenye hatua ya penalti.
Ni tuhuma ambazo hata hivyo zilitupiliwa mbali na kocha wa DRC, Desabre, pia wachambuzi wa soka barani Afrika wakisema Nigeria inapaswa kujilaumu yenyewe na si kutafuta visingizio.
Mathalan, kabla ya kuivaa Gabon, wachezaji wao hawakufanya mazoezi kwa siku mbili kutokana na mgomo wa kushinikiza kulipwa posho zao.
Pia, kwa miaka mitatu ya Desabre akijenga timu, Nigeria imeshuhudia mabadiliko saba ya makocha; Jose Peseiro, Augustine Eguavoen (mara mbili), Finidi George (mara mbili), Emmanuel Amuneke na Chelle.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img