LONDON, Uingereza
KISIWA cha Curacao kimeandika historia ya kuwa taifa dogo zaidi kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia.
Awali, rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Iceland ilipofuzu fainali za mwaka 2018 nchini Urusi.
Hata hivyo, Curacao ni ndogo zaidi kwani nchi hiyo ina watu 150,000, ni sawa na Miji ya Cambridge au Huddersfield ya Uingereza.
Katika mechi 10 za kuwania tiketi, walishinda saba na hawakufungwa hata moja.
Si tu kufuzu, Curacao wamemfukuzisha kazi kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England, Steve McClaren.
McClaren alikuwa kocha wa Jamaica, ambayo ilihitaji ushindi ili kufuzu lakini ikalazimishwa suluhu na Curacao.
Ni mchezo ambao Jamaica walikuwa nyumbani, wakiamini wangefuzu kwa mara ya pili baada ya kucheza michuano hiyo mwaka 1998.
Kikosi cha Curacao kinanolewa na mmoja kati ya makocha wenye heshima kubwa Uholanzi na Ulaya kwa ujumla, Dick Advocaat.
Advocaat ana ‘CV’ ya kuzinoa timu za taifa za Uholanzi, Falme za Kiarabu (UAE), Korea Kusini, Ubelgiji, Urusi, Serbia na Iraq.
Akiwa na Uholanzi mwaka 1994, aliiongoza timu hiyo kufika robo fainali, ingawa Korea Kusini aliyoinoa mwaka 2006 iliishia hatua ya makundi.
Klabu alizowahi kuzinoa ni pamoja na PSV Eindhoven, Rangers, Zenit St Petersburg, Sunderland na Feyenoord.
Alianza kuinoa Curacao mwanzoni mwa mwaka jana na sehemu kubwa ya kikosi chake ni wachezaji walizaliwa Uholanzi.
Baadhi ya mastaa kikosini ni mshambuliaji wa Middlesbrough, Sontje Hansen, na kiungo wa Sheffield United, Tahith Chong, ambaye aliwahi kupita Manchester United.
Advocaat akiwa na umri wa miaka 78, atakwenda Kombe la Dunia akiwa ndiye kocha ‘mzee’ zaidi kuiongoza timu kwenye historia ya michuano hiyo.
Kwa sasa, rekodi hiyo inashikiliwa na Otto Rehhagel, ambaye mwaka 2010, akiwa kocha wa Ugiriki, alikwenda Kombe la Dunia akiwa na miaka 71.
Soka la Curacao linakua kwa kasi. Miaka 10 tu iliyopita, walikuwa nafasi ya 150 kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Kwa sasa ni wa 82.
Msimu huu, Curacao wataunga na Cape Verde, Uzbekistan na Jordan katika orodha ya mataifa manne yanayoshiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
Published:


