18 C
New York

Super Eagles ilivyokwama kufuzu Kombe la Dunia

Published:

LAGOS, Nigeria
LICHA ya kuwa na kikosi chenye mastaa Victor Osimhen, Ademola Lookman na Alex Iwobi, timu ya soka ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ imeshindwa kufuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani.
Eagles haitakuwa sehemu ya timu 48 zitakazoshiriki baada ya kufungwa kwa penalti na DRC katika mchezo wa ‘play-off’ uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taifa linaloshika nafasi ya tano katika viwango vya ubora wa soka barani Afrika, linazikosa fainali za Kombe la Dunia kwa misimu miwili mfululizo baada ya kutokwenda Qatar mwaka 2022.
Hata kabla ya kufungwa na DRC, kambi ya Eagles ilitikiswa na mgomo wa wachezaji na wafanyakazi, wakidai posho zao.
Kuelekea mchezo wao wa kwanza dhidi ya Gabon, wachezaji wa Eagles hawakufanya mazoezi kwa siku mbili kutokana na mgomo huo.
Baada ya Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) kumaliza utata, Eagles walipata ushindi mnono wa mabao 4-1.
Kama itakumbukwa, Nigeria walipangwa Kundi C lililokuwa na Afrika Kusini, Benin, Zimbabwe, Rwanda na Lesotho.
Katika mechi ya kwanza dhidi ya Lesotho, Eagles chini ya kocha Jose Peseiro walitoka sare ya bao 1-1, kabla ya kuambulia tena pointi moja mbele ya Zimbabwe.
Matokeo hayo yalisababisha kocha huyo atimuliwe na nafasi yake kuchukuliwa na winga wa zamani wa Eagles, Finidi George.
Chini yake, matumaini ya kufuzu Kombe la Dunia yalionekana kufifia zaidi baada ya sare dhidi ya Afrika Kusini na kufungwa mabao 2-1 na Benin.
Matokeo hayo yalisababisha Eagles kubaki na pointi tatu tu baada ya mechi nne, hivyo George kufukuzwa na nafasi yake kuchukuliwa na kocha wa sasa, Chelle.
Chelle raia wa Ivory Coast, anakuwa Mwafrika wa kwanza ambaye si raia wa Nigeria kupewa mikoba hiyo ya kuliongoza benchi la ufundi la Eagles.
Kwa muda mfupi, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuirejeshea uhai Eagles, ingawa kikosi hicho hakikuweza kukata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Kwa sasa, Eagles wanaelekeza nguvu katika fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka huu (AFCON 2025) zitakazoanza Desemba, mwaka huu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img