LONDON, Uingereza
UPEPO unavuma vibaya kwa Jonathan Barnett, ambapo wakala huyo wa soka anakabiliwa na mashitaka ya ubakaji mjini London.
Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa mahakamani, Barnett aliyewahi kutajwa na jarida la Forbes kama wakala mwenye ushawishi zaidi duniani, alimbaka mwanamke anayefahamika kwa jina la Jane Doe.
Taarifa zinaeleza kuwa alimsafirisha mwanamke huyo kutoka Australia hadi Uingereza na kisha kumbaka mara 39.
Barnett anatajwa kufanya hivyo mwaka 2017 katika moja ya vyumba vya hoteli aliyokodi jijini London. Alimshikilia mwanamke huyo kwa miaka sita.
Jane ameiambia Mahakama kuwa alianza kujuana na wakala huyo katika miaka ya 1990 kupitia kwa rafiki yake. Walianza kuwasiliana kupitia mitandao, kabla ya kupanga kukutana.
Jane alipofika Uingereza akitokea kwao, Australia, alimtembelea Barnett, siku ambayo anasema alibakwa na wakala huyo wakiwa nyumbani kwake.
Kwa mujibu wake, Barnett alimshawishi kuhamia Uingereza na watoto wake, akiahidi kuwasomesha na kumpa ajira yenye mshahara mnono katika kampuni yake ya uwakala wa soka ya Stellar Group.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Jane, maisha yalikuwa mabaya zaidi akiwa na Barnett kwani haikuwa kubakwa tu, bali pia wakati mwingine alikuwa akimtembezea kichapo.
Baada ya miaka sita ya mateso, waliachana na ndipo wakala huyo alipompa Pauni milioni moja ili kuitunza siri hiyo.
Sasa, ili kujinasua katika kesi hiyo, Barnett amemwajiri wakili maarufu wa mastaa wa soko la filamu za Marekani (Hollywood), Marty Singer.
Aidha, wakala huyo amekiri kuwa yeye na mwanamke huyo, Jane, waliwahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi. Anasema:
“Uhusiano ulipokwisha, alitishia kutangaza uhusiano wetu, akisema angefanya hivyo endapo nisingempa kiasi cha fedha.
“Kutokana na vitisho hivyo, nililazimika kumlipa fedha kwa miaka mingi, nikiwa nimeshamlipa Pauni 1,000,000.”
Barnett ni mmiliki wa kampuni ya uwakala wa soka ya Stellar Group. Ilianzishwa mwaka 1992 na ni moja ya kampuni maarufu katika ulimwengu wa kandanda.
Kampuni hiyo ilijipatia umaarufu zaidi mwaka 2013 baada ya kusimamia dili la Gareth Bale kujiunga na Real Madrid akitokea Tottenham, usajili uliogharimu kitita cha Pauni milioni 85.
Mbali ya Bale, kampuni hiyo pia imekuwa ikiwasimamia wachezaji wengi maarufu, wakiwamo Jack Grealish, Ivan Toney, Jordan Pickford na Ruben Loftus-Cheek.
Published:


