15.2 C
New York

Joshua, Paul nani kupigwa ‘KO’?

Published:

LONDON, Uingereza
BAADA ya tetesi nyingi na za muda mrefu, sasa ni rasmi kuwa Anthony Joshua na Jake Paul watapanda ulingoni kurushiana makonde.
Ni pambano la raundi nane litakalopigwa Desemba 19, mwaka huu. Awali, Paul alitarajiwa kuzichapa na Gervonta Davis, kabla ya mwenzake huyo kujitoa baada ya kufunguliwa mashitaka ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya aliyewahi kuwa mpenzi wake.
Joshua mwenye umri wa miaka 36, akiwa na uzoefu wa miaka 12 katika ngumi za kulipwa, ana rekodi ya kupigana mapambano 32, akishinda 28 (25 kwa KO) na kupigwa manne.
Kwa nyakati tofauti, ameshinda mikanda ya WBA, IBF, WBO na IBO, pia akiwahi kutwaa medali ya dhahabu katika michuano ya Olimpiki mwaka 2012.
Mapambano makubwa aliyowahi kushinda na kumpa heshima kubwa katika ulimwengu wa masumbwi ni dhidi ya Kubrat Pulev (2020), Andy Ruiz Jr. (2019), Alexander Povetkin (2018) na Klitschko (2017).
Mara ya mwisho kwa Joshua kupanda ulingoni ilikuwa Septemba, mwaka jana, ambapo alipigwa na Muingereza mwenzake, Daniel Dubois, kwa KO ya raundi ya tano.
“Nilikuwa kimya muda mrefu. Nilitumia muda mwingi kuhakikisha narudi kufanya makubwa. Hii ni nafasi muhimu kwangu,” amesema Joshua.
Kwa upande wake, Paul ana mapambano 13, ambapo ameshinda 12 (7 kwa KO) na kupigwa mara moja. Mara yake ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Juni, mwaka huu, ambapo alishindwa kwa pointi mbele ya Julio Cesar Chavez Jr.
Kabla ya kukutana na Chavez Jr, itakumbukwa kuwa Paul alimtandika nguli wa ngumi za uzito wa juu nchini Marekani, Mike Tyson.
“Nitakapomdunda Anthony Joshua, nitakuwa nimewanyamazisha wale wote wanaobeza uwezo wangu. Hicho ndicho ninachopaswa kuwapa wale wote wanaonichukia,” anasema Paul mwenye umri wa miaka 28.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img