15.2 C
New York

Haaland na safari yake ya kwanza Kombe la Dunia 2026

Published:

MANCHESTER CITY, Uingereza
NDOTO imetimia! Mshambuliaji wa kati wa Manchester City, Erling Haaland, atacheza kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia wakati timu yake ya taifa ya Norway itakaposhiriki fainali hizo hapo mwakani.
Norway imekata tiketi, huku Haaland akiwa na mchango mkubwa wa mabao 16 katika mechi nane za kufuzu. Mabao 12 katika michezo minne ya mwisho.
Ni kwa maana hiyo, si tu ameiwezesha Norway kukata tiketi, bali pia Haaland mwenye umri wa miaka 25 ndiye mfungaji bora wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia.
Katika mchezo wao wa mwisho wikiendi iliyopita, ambapo waliifunga Italia mabao 4-1, Haaland aliingia kambani mara mbili.
Licha ya kwamba itakuwa ni mara yao ya nne kucheza Kombe la Dunia, Norway haijashiriki michuano yoyote mikubwa tangu ilipokuwa kwenye fainali za Mataifa ya Ulaya (EURO) mwaka 2000.
“Hatujawahi kuwa na mchezaji wa kiwango cha juu kama alivyo Erling (Haaland). Hakuna ubishi kuwa ndiye mchezaji mkubwa zaidi kuwahi kutokea (Norway),” anasema mwandishi wa habari nchini Norway, Lars Sivertsen.
Rekodi ya Haaland katika timu ya taifa inavutia mno. Nyota huyo wa zamani wa Borussia Dortmund ameifungia mabao 55 katika mechi 48 alizocheza.
Kwa ujumla, ukiweka na mechi alizocheza katika klabu yake ya Man City, Haaland ameshazifumania nyavu mara 32 katika mechi 20 tu alizocheza msimu huu.
Hata hivyo, katika kikosi cha Norway, pia kuna kiungo wa Arsenal, Martin Odegaard, ambaye ndiye mchezaji mwenye ‘asisti’ nyingi zaidi (7) katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia kwa upande wa Ulaya.
Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid, ambaye ana umri wa miaka 26, amecheza mechi 67 tangu alipoanza kuitwa kwenye kikosi cha Norway akiwa na umri wa miaka 15.
Norway imewahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia mara tatu (1938, 1994 na 1998), pia ikicheza michuano ya Euro mwaka 2000.
Baba yake Haaland, Alf Inge, alikuwa sehemu ya kikosi kilichocheza Kombe la Dunia mwaka 1994 na aliwahi kupita katika klabu za Nottingham Forest, Leeds na Manchester City, ingawa hakuwahi kubeba taji lolote.
Kubwa zaidi kwa Haaland ni kwamba sasa ameepuka kuingia kwenye orodha ya wachezaji wakubwa waliokosa kucheza Kombe la Dunia katika maisha yao ya soka.
Kwa sasa, orodha hiyo ina George Weah, George Best, Alfredo di Stefano, Laszlo Kubala, Gunnar Nordahl, Ryan Giggs na Ian Rush.
Weah, licha ya kuwika Ulaya, ikiwamo kuwa Mwafrika pekee kuwahi kubeba tuzo ya Ballon d’Or, na kucheza Monaco, PSG, AC Milan na Chelsea, hakuwahi kuiwakilisha Liberia katika michuano ya Kombe la Dunia.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img