14 C
New York

Wezi wanavyowanyima raha wanasoka Ulaya

Published:

LONDON, Uingereza
TUKIO la Raheem Sterling kuvamiwa na majambazi akiwa na familia yake nyumbani limetikisa vyombo vya habari barani Ulaya, ikiwa ni mara ya pili kwa winga huyo kukutwa na majanga hayo.
Mwaka 2022, wakati akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya England kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar, Sterling alilazimika kurudi England baada ya taarifa za wezi kuingia nyumbani kwake.
Hata hivyo, Sterling si mchezaji wa kwanza na pekee kuwahi kuingia kwenye changamoto hiyo ya kuvamiwa na majambazi katika makazi yake.
Kama itakumbukwa, beki raia wa Sweden, Victor Lindelof, aliwahi kukutwa na majanga hayo alipokuwa mchezaji wa Manchester United.
Akiwa uwanjani siku ambayo Man United ilikuwa ikimenyana na Brentford, wezi waliingia nyumbani kwake na kumkuta mkewe, Maja, akiwa na watoto wao wawili.
“Nilikuwa nyuumbani na watoto. Tulilazimika kujificha kwenye chumba kimoja baada ya kugundua tumevamiwa na wezi. Hakuna aliyedhurika, lakini ilituogopesha sana,” alisimulia Maja.
Kupitia utafiti wake, Shirika la Habari la VICE World News linabaini kuwa matukio ya wachezaji wenye majina makubwa kuvamiwa na wezi yameongezeka kwa kasi tangu miaka ya 2000.
Ni kipindi hicho, ndipo mchezaji wa kandanda alianza kulipwa mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki, fedha ambazo ni nyingi na zinawavutia majambazi. Tangu kipindi hicho, mastaa wa soka zaidi ya 80 wameripotiwa kuvamiwa majumbani mwao.
Miaka michache iliyopita, aliyekuwa beki wa Manchester City, Joao Cancelo, alivamiwa na wezi wanne akiwa nyumbani na familia yake.
Tukio hilo lilifuatiwa na lile la staa wa Chelsea, Reece James, ambaye wezi walipoingia ndani kwake waliondoka na vitu vya thamani, ikiwamo medali yake ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Nje ya England, Karim Benzema anaweza kuwa na bahati mbaya zaidi. Akiwa mchezaji wa Real Madrid wakati huo, alivamiwa mara tatu kwa nyakati tofauti.
Haijasahaulika pia kuhusu Angel Di Maria. Akiwa PSG, alilazimika kutolewa uwanjani katika mchezo dhidi ya Nantes ili arudi nyumbani kuiwahi familia yake iliyokuwa imevamiwa na wezi.
Kama itakumbukwa, siku hiyo pia, mchezaji mwenzake katika kikosi cha PSG, Marquinhos, naye alikutwa na mkasa wa nyumba yake kuvamiwa.
Ni baada ya tukio hilo la wezi, Di Maria aliamua kuiuza moja kwa moja nyumba hiyo yenye thamani ya Pauni milioni nne na kuihamishia familia yake hotelini.
Nyota wengine wa kandanda waliowahi kuingia kwenye mtego wa majambazi ni Julian Draxler, Dele Alli, Jan Vertonghen, Frank Lampard,
Swali ni je, katika mazingira ya ulinzi mkali kwenye nyumba za mastaa, zikiwamo kamera na mbwa wenye mafunzo, inakuwaje bado wanaishi kwa hofu ya kuvamiwa na wezi?
Tafiti zinaonesha kuwa matukio ya aina hiyo hufanywa na wezi wenye weledi mkubwa, wakihusishwa na mafunzo kutoka katika magenge makubwa ya uhalifu.
Katika hao, anatajwa Alfredo Lindley ‘Lupin’, ambaye ni mwizi wa madini anayefahamika mno nchini kwao, Ufaransa. Lupin ndiye aliyesuka mpango wa kuvamia nyumba ya Lampard jijini London, wakati huo akiwa kocha wa Chelsea.
Hata hivyo, ipo dhana kuwa wapo wachezaji wanaoshirikiana na wezi kwa kuwapa taarifa muhimu juu ya nyumba za wenzao na namna ya kuingia.
“Utakuta katika baadhi ya matukio, wezi wanakwenda moja kwa moja kwenye eneo la siri, ambalo kuna vitu vya thamani. Hii inamaanisha nini? Wamepewa taarifa na mtu aliye karibu na mchezaji,” anasema mmoja ya viongozi wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa nchini Uingereza.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img