LAGOS, Nigeria
TIMU ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ imeingia fainali ya hatua ya mtoano (playoffs) ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani katika mataifa ya Marekani, Canada na Mexico.
Katika mchezo uliochezwa Morocco, Eagles waliifunga Gabon mabao 4-1 na sasa wanaisubiri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyoifunga Cameroon katika mchezo mwingine wa ‘playoff’.
Mshindi kati ya Eagles na DRC katika mtanange huo wa fainali ataungana na timu zingine tisa zilizokata tiketi ya kuiwakilisha Afrika katika fainali hizo.
Dhidi ya Gabon, straika wa Galatasaray, Victor Osimhen, aliendelea kuibeba Eagles kama ambavyo amekuwa akifanya katika siku za hivi karibuni.
Osimhen, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uturuki msimu uliopita, alifunga mabao mawili, huku Chidera Ejuke na Akor Adams nao wakizifumania nyavu za Gabon.
Nyota huyo amefikisha mabao 31 akiwa na kikosi cha Eagles, akibakiza sita pekee kumfikia mfungaji bora wa muda wote, Rashidi Yekini.
Katika safari ya kuisaka tiketi ya kwenda Kombe la Dunia hapo mwakani, Osimhen amehusika katika mabao 14.
Takwimu zinaonesha kuwa Eagles haijafungwa katika mechi zote nane alizoweza kufunga bao. Wameshinda sita na kupata sare mbili.
Aidha, katika mechi 22 alizocheza hivi karibuni, zikiwamo za fainali za AFCON, Eagles imeshinda 15, imefungwa tatu na kupata sare nne.
Ikumbukwe, hata Eagles ilipofuzu fainali za AFCON mwaka 2021 na 2023, Osimhen ndiye aliyekuwa shujaa wao, akitwaa tuzo ya mfungaji bora.
Published:


