Na mwandishi wetu, Gazetini
SOKA la wanawake nchini Korea ya Kaskazini limepata mafanikio makubwa katika miaka ya hivi karibuni, ambapo timu yake ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 imetoka kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia, ikifanya hivyo kwa misimu miwili mfululizo.
Korea ya Kaskazini imetwaa taji hilo msimu huu kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uholanzi, michuano hiyo ikimalizika hivi karibuni nchini Morocco.
Ikiwa ni mara yao ya nne kuwa mabingwa, vijana hao waliruhusu mabao matatu pekee katika mashindano hayo. Katika mechi nne, walifunga mabao matatu au zaidi.
Mafanikio ya U-17 yanakuja baada ya vijana wenzao wenye umri chini ya miaka 20 (U-20) kuwa mabingwa wa Kombe la Dunia, hiyo ikiwa ni mara ya nne kwao kufanya hivyo.
Walipotwaa ubingwa huo mwaka 2024, U-20 ya Korea ya Kaskazini iliifunga Argentina mabao 6-2 na kupata ushindi wa bao 1-0 kuanzia robo fainali.
Je, nini siri ya mafanikio hayo ya soka la wanawake nchini Korea ya Kusini, hasa kwa timu zake za vijana? Makala haya yanachambua.
Baada ya kuona si rahisi kufikia maendeleo ya Ligi kubwa za Ulaya za soka la wanaume za barani Ulaya, Korea ya Kaskazini iliamua kuwekeza zaidi kwa upande wa wanawake.
Kwa Korea ya Kaskazini, Serikali imewekeza fedha nyingi katika programu maalumu ya Serikali inayosimamia vipaji vya soka kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka 13.
Ifahamike kuwa programu hiyo ya Serikali imekuwa ikiwafikia hata mabinti wanaoishi maeneo ya vijijini, ambako maisha ni magumu kwa familia zilizo nyingi.
Kupitia programu hiyo, mabinti wenye vipaji vya soka huchukuliwa na kufadhiliwa masomo, pamoja na kupangiwa nyumba za kuishi katika maeneo ya mjini ili kuweza kutimiza ndoto zao za kucheza kandanda.
Matokeo ya jitihada hizo za Serikali ni Korea ya Kaskazini kuzalisha mastaa kama Yu Jong-hyang aliyekuwa mfungaji bora wa msimu huu wa fainali za Kombe la Dunia za U-17.
Published:


