MERSEYSIDE, Uingereza
LIVERPOOL iko taabani. Vipigo vitano katika mechi 11 walizocheza hivi karibuni. Kwa mujibu wa kocha wake, Arne Slot, bado ni mapema kuitoa Liverpool katika mbio za ubingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Hata hivyo, licha ya Slot kuamini bado wana nafasi, timu yake iko nafasi ya nane katika msimamo wa EPL, ikiwa imecheza mechi 11 na kukusanya pointi 18 pekee. Wamezidiwa pointi nane na Arsenal iliyokaa kileleni.
Matumaini yalionekana kufifia zaidi baada ya kiwango kibovu walichokionesha katika kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Manchester City.
Kwa upande wake, makala haya yanaangazia changamoto zinazoikabili Liverpool msimu huu wa EPL na mashindano mengine.
Usajili wa Wirtz haujalipa
Liverpool ilitumia Pauni milioni 116 kumsajili Florian Wirtz akitokea Bayer Leverkusen. Ni usajili uliovunja rekodi ya usajili Anfield, kabla ya Alexander Isak kusajiliwa.
Usajili wa bei mbaya wa Wirtz ulitokana na kiwango bora alichokuwa nacho Bundesliga, ambapo Mjerumani huyo alifunga mabao 34 na kutoa ‘asisti’ 35 kwa misimu miwili aliyocheza Leverkusen.
Hata hivyo, Wirtz mwenye umri wa miaka 22 hajaweza kuhamishia makali yake Anfield. Hajaziona nyavu wala kutoa asisti katika mechi alizocheza EPL.
Kiwango cha Konate
Msimu uliopita, Ibrahima Konate alitengeneza ‘pacha’ nzuri ya nafasi ya beki wa kati kwa kushirikiana na Virgil van Dijk. Konate alikuwa mwepesi kunusa, kuondosha hatari na hata kuanzisha mashambulizi.
Msimu huu, mambo ni tofauti. Katika mechi dhidi ya Man City, alisababisha penalti aliyokosa Erling Haaland. Kama hiyo haitoshi, makosa yake yalimpa Haaland bao la kuongoza kwa upande wa Man City.
Itakumbukwa, kiwango chake kibovu pia kilisababisha Liverpool kupoteza mechi dhidi ya Crystal Palace, Galatasaray na Brentford.
Majeraha
Hii ni sababu nyingine kubwa ya anguko la Liverpool kwa sasa. Kwa nyakati tofauti, kocha Slot amekuwa akiwakosa baadhi ya nyota wake muhimu.
Mfano; mlinda mlango namba moja wa kikosi, Alisson, amekosekana katika mechi nane mfululizo za hivi karibuni.
Nyota mpya, Giovanni Leoni, alipata majeraha katika mechi yake ya kwanza tu. Wakati fulani, Alexis Mac Allister, naye haikuwa dimbani. Ni kama ilivyo kwa Curtis Jones.
Published:


