DOHA, Qatar
LIGI Kuu ya Qatar kwa sasa ni nyumbani kwa mastaa wengi wa soka waliowahi kutamba katika soka la Ulaya wakiwa na klabu mbalimbali, zikiwamo Liverpool na Real Madrid.
Ujio wa wachezaji hao wenye majina makubwa ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Qatar hata kabla ya nchi hiyo kuandaa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2022.
Aleksandar Mitrovic
Mshambuliaji wa kati huyo wa zamani wa Fulham ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa sasa anaitumikia Al-Rayyan ya Qatar.
Alitua Qatar alipojiunga na Al Hilal, ambayo aliifungia mabao 68 katika mechi 79, kabla ya kusajiliwa na wapinzani wao, Al-Nassr. Ameshaifungia mabao mawili katika mechi tatu tu.
Marco Verratti
Miaka michache iliyopita, nyota huyo raia wa Italia alikuwa mmoja ya viungo bora katika soka la Ulaya. Aliondoka PSG mwaka 2023.
Kwa sasa, Verratti ni mchezaji wa Al Duhail iliyomsajili akitokea kwa wapinzani wao, Al-Arabi. Staa huyo ana umri wa miaka 33, hivyo huenda akarudi kukipiga barani Ulaya.
Roberto Firmino
Firmino alitimkia Qatar majira ya kiangazi baada ya miaka miwili ya kukipiga Ligi Kuu ya Saudi Arabia. Mbrazil huyo alisajiliwa Saudi baada ya misimu nane akiwa na Liverpool.
Nyota huyo anaitumikia Al Sadd ya Ligi Kuu nchini Qatar, ambapo ameshafunga mabao sita katika mechi nane. Hivi karibuni, alipachika ‘hat-trick’ walipopata ushindi wa mabao 8-0.
Julian Draxler
Kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani alijiunga na Al-Ahli ya Qatar mwaka 2023. Ameshahusika katika mabao 40 kwa mechi 50 pekee alizocheza.
Akiwa na umri wa miaka 32 tu kwa sasa, bado Draxler ana uwezo wa kucheza soka la ushindani barani Ulaya.
Presnel Kimpembe
Miaka miwili ya mwishoni mwa maisha yake katika kikosi cha PSG yalitawaliwa na wimbi la majeraha ya mara kwa mara.
Nyota huyo raia wa Ufaransa alilazimika kufanyiwa upasuaji wa mara kwa mara, kabla ya kuamua kujiunga na Qatar SC.
Published:


