MADRID, Hispania
ALIWAHI kutabiriwa kuwa staa mpya wa soka la Brazil, akitajwa kufuata nyayo za mastaa wengi waliwahi kupiga katika ardhi ya nchi hiyo, wakiwamo Ronaldinho, Robinho, Kaka na Neymar.
Msimu wake wa kwanza baada ya kujiunga na Real Madrid, Endrick mwenye umri wa miaka 19 alianza vizuri, ambapo alicheza mechi 37 lakini sasa amekuwa mchezaji wa benchi tangu kocha Xabi Alonso alipoajiriwa.
Msimu huu, Endrick amecheza dakika 14 pekee, tena akitokea benchi katika mchezo dhidi ya Valencia. Madrid ilishinda mabao 4-0.
Kutokana na kushindwa kupata nafasi katika klabu yake, ‘dogo’ huyo amepoteza namba kwenye kikosi cha Brazil. Kocha Carlo Ancelotti ameamua kumfungia mlango.
Hii inaashiria kwamba nafasi ni finyu mno kwa Endrick kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa na mataifa ya Marekani, Canada na Mexico.
Usajili wake Santiago Bernabeu
Endrick alijiunga na Madrid mwaka jana, siku chache tu baada ya kutimiza umri wa miaka 18. Alitua Santiago Bernabeu kwa kitita cha Pauni milioni 63 akitokea Palmeiras ya Ligi Kuu nchini Brazil.
Wakati anasajiliwa, tayari mshambuliaji huyo alishaifungia Brazil jumla ya mabao matatu katika mechi 10.
Chini ya Ancelotti aliyekuwa kocha wa Madrid wakati huo, Endrick alifunga mabao saba katika msimu wake wa kwanza Bernabeu.
Hata hivyo, majeraha aliyopata Mei, mwaka jana, yalimrudisha dimbani Septemba 20, mwaka huu. Tangu hapo, Endrick hajaweza kuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha Madrid.
Chelsea kumnasa Januari?
Kuelekea usajili wa dirisha dogo la Januari, mwakani, taarifa nyingi zinamuhusisha Endrick na mpango wa kuondoka kwa mkopo.
Chelsea, West Ham na Aston Villa ya kocha wa zamani wa Arsenal, Unai Emery, ni miongoni tu mwa klabu zinazoripotiwa kuitolea macho saini yake kuelekea Januari.
Licha ya kutakiwa Ligi Kuu ya England, pia zipo tetesi kuwa klabu ya Lyon, ambayo msimu huu inashiriki Ligi ya Europa, nayo inajaribu kuinasa saini ya nyota huyo.
Lakini, Januari, mwaka huu, Endrick alihusishwa na mpango wa kuondoka Madrid lakini klabu hiyo iligoma kufanya biashara. Nyota huyo pia alionesha kuwa anataka kubaki.
Published:


