Na mwandishi wetu, Gazetini
NI msimu wa 35 wa fainali za Mataifa Afrika (AFCON) na michuano hiyo itafanyika Kaskazini mwa Afrika katika Taifa la Morocco.
Msimu uliopita wa michuano hiyo uliishuhudia Ivory Coast ikiwa mwenyeji ikinyakua ubingwa kwa kuifunga Nigeria katika mchezo wa fainali.
Itakuwa ni mara ya pili kwa Morocco kuandaa mashindano hayo baada ya kuwa mwenyeji mwaka 1988. Safari hii, ilipata fursa hiyo ikuchukua nafasi ya Guinea iliyokwama kwenye maandalizi.
Fainali hizo zitaanza lini?
Michuano ya AFCON 2025 itaanza Desemba 21 na kufikia ukomo Januari 18, mwaka huu. Mechi zitachezwa katika miji sita ya Rabat, Casablanca, Tangier, Fes, Agadir, Marrakesh.
Mfumo wa mashindano ukoje?
AFCON 2025 itashirikisha timu 24, ambazo zitawekwa katika makundi sita (timu nne kila kundi). Timu mbili katika kila kundi nitaingia hatua ya 16 bora na kuungana na nne zitakazofanya vizuri katika nafasi ya tatu kila kundi.
Lipi ni kundi la kifo?
Kundi A: Comoro, Mali, Morocco, Zambia. Kundi B: Angola, Misri, Afrika Kusini, Zimbabwe. Kundi C: Nigeria, Tanzania, Tunisia, Uganda.
Kundi D: Benin, Botswana, DR Congo, Senegal. Kundi E: Algeria, Burkina Faso, Guinea ya Ikweta, Sudan. Kundi F: Cameroon, Gabon, Ivory Coast na Msumbiji.
Morocco kubakiza Kombe nyumbani?
Wachambuzi wengi wa soka barani Afrika wanaipa nafasi kubwa Morocco kutokana na faida ya kuwa nyumbani katika michuano hiyo.
Pia, Taifa hilo linafanya vizuri katika soka, ambapo kwa sasa linashika nafasi ya kwanza barani Afrika na ya 12 kwenye viwango vya ubora duniani.
Chini ya kocha wake, Walid Regragui, kikosi hicho kina wachezaji wanaowika katika ulimwengu wa kandanda, wakiwamo Achraf Hakimi, Yassine Bounou, Hamza Igamane na Hakim Ziyech.
Hata hivyo, msimu uliopita wa AFCON ya mwaka 2023, Morocco iliishia hatua ya 16 bora, ambapo walitolewa na Ivory Coast iliyotwaa ubingwa.
Ivory Coast ina nafasi ya kutetea ubingwa?
Ndiyo, wanaweza kutetea ubingwa wao, hasa baada ya kiwango kizuri walichokionesha katika mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwakani?
Wakiwa na kocha mzawa, Emerse Fae, Ivory Coast walikata tiketi wakiwa hawajapoteza mchezo, pia safu yao ya ulinzi ikiwa haijaruhusu bao katika mechi nne.
Lakini, pia kuna Senegal, ambayo kikosi chake kina mastaa Edouard Mendy, Sadio Mane, Nicolas Jackson, Pape Mate Sarr, Pape Gueye na Idrissa Gana Gueye, nayo inapewa nafasi ya kutwaa ubingwa.
Ni kama ilivyo kwa Misri ya Mohamed Salah, ambayo ina historia ya kutwaa mara saba taji hilo la AFCON na haijafungwa tangu Machi, mwaka jana.
Kikosi hicho cha kocha Hossam Hassan kimefunga mabao tisa katika mechi sita zilizopita, pia hakijaruhusu nyavu zake kutikiswa.
Nigeria iliyofika fainali mwaka 2023 na kufungwa na Ivory Coast, nayo si ya kubeza msimu huu wa AFCON kwani Ina kikosi chenye baadhi ya nyota tishio, wakiwamo Victor Osimhen, Ademola Lookman, Akor Adams na Tolu Arokodare.
Published:


