23.2 C
New York

Makinda watakaowasha moto AFCON 2025

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
KWA miaka mingi, fainali za Mataifa Afrika (AFCON) zimekuwa zikiibua vipaji vipya vya soka, kama ilivyowahi kutokea kwa Samuel Eto’o, Yaya Toure, Mohamed Salah na Victor Osimhen.
Msimu huu, michuano hiyo itaanza Desemba na kumalizika Januari, mwakani, ambapo mwenyeji wake ni Morocco.
Ikiwa imebaki takribani miezi miwili tu, wapo wachezaji wenye umri mdogo wanaotarajiwa kuyababe mataifa yao na kujitangaza zaidi katika ulimwengu wa soka.
Mamadou Lamine Camara (Senegal, RS Berkane)
Chini ya kocha Pape Thiaw, Camara alianza kuitumikia timu ya wakubwa ya Senegal mwaka 2023, wakati huo akiwa na umri wa miaka 20 tu.
Nyota huyo atakwenda katika fainali za mwaka huu akiwa tayari amekomaa zaidi baada ya kucheza mechi tano za ‘Simba wa Teranga’. Amefunga bao moja.
Karim Konate (Ivory Coast, RB Salzburg)
Ni moja ya vipaji vikubwa vya soka barani Afrika. Konate ameshafunga mabao mawili tangu alipoanza kuitwa kwenye timu ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 17 tu.
Alithibitisha uwezo wake baada ya kuzifumania nyavu katika mechi zilizopita za kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia.
Amad Diallo (Ivory Coast, Man United)
Diallo alianza kuitumikia timu ya wakubwa mwaka 2013 chini ya kocha Patrice Beaumelle, wakati huo akiwa na umri wa miaka 18.
Diallo, kiungo wa pembeni anayekipiga katika klabu ya Manchester United, ameshafunga mabao mawili akiwa na kikosi hicho cha Ivory Coast.
Oussama Targhalline (Morocco, Feyenoord)
Targhalline alianza kucheza timu ya wakubwa mwaka jana, wakati huo akiwa na umri wa miaka 22. Kocha aliyempa nafasi hiyo ni Walid Regragui.
Nyota huyo ameshacheza mechi saba na tayari ni kipenzi cha mashabiki wa Morocco kutokana na uwezo na utulivu wake mkubwa kwenye eneo la kiungo.
Noah Sadiki (DRC, Sunderland)
Kocha raia wa Ufaransa, Sebastien Desabre, alianza kumwita kwenye kikosi cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Sadiki ameshacheza mechi 11 akiwa na kikosi hicho na ni mmoja ya wachezaji wenye umri mdogo wanaotazamiwa kufanya vizuri msimu huu wa AFCON.
Benjamin Frederick (Nigeria, Brentford)
Chini ya kocha Eric Chelle, Frederick anayecheza eneo la beki wa kati alianza kujumuhishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’.
Kwa sasa, kinda huyo ni mchezaji wa kikosi cha kwanza na alicheza mechi tano na zote kumaliza dakika 90 katika kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Related articles

Recent articles