Na mwandishi wetu, Gazetini
JUMLA ya timu 16 zimeshaingia hatua ya makundi ya msimu huu wa 2025-26 wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kinachosubiriwa kwa hamu sasa ni droo ya makundi itakayochezeshwa Novemba 3, mwaka huu, mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Waarabu bado wanasumbua
Timu za mataifa ya Afrika ya Kaskazini zimeendelea kuwa na nguvu kubwa kwenye michuano hii ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Wakali wa Morocco, Wydad Casablanca, waliingia makundi kwa ushindi mnono wa jumla ya mabao 6-1 dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana.
Wenzao wa Morocco, OC Safi, waliingia makundi kwa mara ya kwanza baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Stade Tunisien ya Tunisia.
Misri nayo itawakilishwa na timu mbili kwenye makundi, ambazo ni Zamalek SC na Al Masry.
Zamalek SC walikata tiketi ya makundi kwa kuifunga Dekedda ya Somalia jumla ya mabao 7–0.
Kwa upande wao, Al Masry waliiondosha Al-Ittihad ya Libya kwa kichapo cha jumla ya mabao 2–1.
Algeria pia ina timu mbili; USM Alger, ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho mwaka 2023, na
CR Belouizdad.
Kaizer Chiefs wamerudi kibabe
Historia inakumbusha kuwa ni miaka 12 tangu Kaizer ilipogusa hatua ya makundi. Ilikuwa mwaka 2013, ambapo walifika hadi hatua ya 16 bora.
Safari hii, chini ya kocha wa zamani wa Yanga, Cedric Kaze, wameingia makundi kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya AS Simba ya DRC.
Katika hatua hii ya makundi, Afrika Kusini inawakilishwa pia na Stellenbosch FC, ambayo imefika hatua hii ya makundi kwa jasho la kuitoa moja ya timu bora, 15 de Agosto ya Angola.
Azam, Singida BS zitatoboa?
Bendera ya Tanzania inapeperushwa na timu mbili pia kwenye hatua ya makundi, ambazo ni Azam FC na Singida Black Stars.
Matajiri wa Chamazi, Azam, waliitoa KMKM ya Visiwani Zanzibar kwa kichapo cha jumla ya mabao 9–0, wakati Singida BS waliing’oa Flambeau du Centre ya Burundi.
Je, baada ya timu zote hizo kuingia makundi kwa mara ya kwanza, zitavuka hapo na kuingia hatua ya 16 bora?
Timu zingine zinazosubiri kwa hamu droo ya makundi ni USM Alger na CR Belouizdad (Algeria), ZESCO United (Zambia), Maniema Union (DRC), na San Pedro (Ivory Coast), Nairobi United (Kenya), AS Otoho (Congo), na Djoliba (Mali)
Published:


