24.8 C
New York

Afrika na safari ya Kombe la Dunia 2026 (7) – Afrika Kusini

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
MATAIFA tisa ya Afrika yameshajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Tunisia, Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Morocco.
Makala haya yanawaangazia wawakilishi hao wa soka la Afrika kwa kuichambua Afrika Kusini. Je, ina nafasi ya kufanya vizuri Kombe la Dunia?
Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ walilazimika kusubiri hadi mechi ya mwisho kujihakikishia nafasi. Waliifunga Rwanda mabao 3-0. Wanarejea Kombe la Dunia baada ya kuikosa michuano hiyo tangu mwaka 2010.
Chini ya kocha Hugo Broos, Afrika Kusini walipaswa kufuzu tangu Septemba, mwaka huu, lakini walipokonywa pointi tatu baada ya kumchezesha mchezaji mwenye adhabu katika mchezo wao dhidi ya Lesotho.
Zikiwa zimebaki mechi mbili za kufuzu, Afrika Kusini ikajikuta ikiwa nafasi ya pili kwa tofauti ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Benin iliyokuwa inaongoza Kundi.
Katika mechi mbili hizo, Afrika Kusini ilitakiwa kucheza na Zimbabwe na Rwanda, wakati Benin walikuwa na kibarua cha kuzikabili Rwanda na Nigeria.
Zimbabwe haikuwa na uwanja, hivyo mechi yake ya nyumbani ilichezwa Afrika Kusini. Ikamalizika kwa timu hizo kutoka suluhu (0-0).
Baada ya Benin kuifunga Rwanda bao 1-0, mambo yakawa nagumu zaidi. Timu tatu – Afrika Kusini, Benin na Nigeria – zikawa na uwezo wa kufuzu kuelekea mechi za mwisho.
Kwa upande wake, Afrika Kusini ilipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Rwanda. Benin walikubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Nigeria, mchezo ambao Victor Osimhen alipachika ‘hat-trick’.
Hii inakuwa mara ya nne kwa Afrika Kusini kushiriki Kombe la Dunia baada ya kufanya hivyo mwaka 1998, 2002 na 2010, lakini haijawahi kuvuka hatua ya makundi.
Je, ni wakati sasa wa Afrika Kusini kuwika katika michuano hiyo baada ya miaka mingi ya timu yake ya taifa na klabu zake kufanya vizuri barani Afrika?

Related articles

Recent articles