24.8 C
New York

Afrika na safari ya Kombe la Dunia 2026 (5) – Algeria

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
MATAIFA tisa ya Afrika yameshajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Tunisia, Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Morocco.
Makala haya yanawaangazia wawakilishi hao wa soka la Afrika kwa kuichambua Algeria. Je, ina nafasi ya kufanya vizuri Kombe la Dunia?
Algeria walikata tiketi Oktoba 9, mwaka huu, baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Somalia. Licha ya kwamba Somalia walikuwa wenyeji, mechi ilichezwa Algeria. Somalia haina uwanja uliokidhi vigezo vya CAF.
Ikumbukwe, Algeria walifuzu wakiwa na mchezo mmoja mkononi baada ya kukaa kileleni mwa Kundi G na hii inakuwa mara ya tano kwao kucheza Kombe la Dunia, ingawa ni ya kwanza kufuzu tangu mwaka 2014.
Chini ya kocha Vladimir Petkovic, nahodha wake, Riyad Mahrez, ni miongoni mwa silaha za kikosi hicho. Dhidi ya Somalia, nyota huyo alifunga bao moja na kutoa ‘asisti’ mbili.
Mbali ya Mahrez, Algeria inaye Mohamed Amoura. Mshambuliaji huyo wa Wolfsburg ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), ndiye kinara wa mabao katika mechi za kufuzu barani Afrika akiwa ameingia kambani mara 10.
Katika mechi ya mwisho waliyoshinda 2-1 dhidi ya Uganda, Amoura ndiye aliyefunga mabao yote na kuiwezesha Algeria kufikisha pointi 25. Ilifuzu ikiwa imeshinda mechi nane, imefungwa moja na kutoa sare moja.
Petkovic ni kocha aliyeajiriwa kuziba pengo la Djamel Belmadi, ambaye aliondoka Januari, mwaka jana, baada ya Algeria kutolewa mapema kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
Ni mara ya pili kwa kocha huyo raia wa Uswis kufuzu Kombe la Dunia baada ya kushiriki michuano hiyo akiwa mkuu wa benchi la ufundi la timu yake ya taifa mwaka 2018.
Licha ya kwamba hii ni mara ya tano kushiriki, ni mara moja tu Algeria ilifanikiwa kuvuka makundi. Ni mwaka 2014, ambapo waliondoshwa na Ujerumani katika hatua ya mtoano (16 bora).

Related articles

Recent articles