24.8 C
New York

Afrika na safari ya Kombe la Dunia 2026 (4) – Ghana

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
MATAIFA tisa ya Afrika yameshajihakikishia tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico. Tunisia, Algeria, Ghana, Misri, Senegal, Afrika Kusini, Ivory Coast, Cape Verde na Morocco.
Makala haya yanawaangazia wawakilishi hao wa soka la Afrika kwa kuichambua Ghana. Je, ina nafasi ya kufanya vizuri Kombe la Dunia?
Ghana ‘Black Stars’ wanashiriki kwa mara ya tano. Walikata tiketi baada ya ushindi wa mbinde wa bao 1-0 katika mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Comoro. Mohammed Kudus ndiye aliyepachika, likiwa ni bao lake la pili katika mechi za kufuzu.
Safari hii, walikata tiketi wakiwa kileleni mwa msimamo wa Kundi I baada ya kukusanya pointi 25 katika mechi 10, walifunga jumla ya mabao 23.
Nahodha wa kikosi, Jordan Ayew, amekuwa kwenye kiwango bora, ambapo alifunga mabao saba na kutoa ‘asisti’ saba. Hizi zitakuwa ni fainali za tatu za Kombe la Dunia kwa nyota huyo wa Leicester City.
Hivyo, Ayew anaungana na Asamoah Gyan, Sulley Muntari na Andre Ayew katika orodha ya wachezaji wa Ghana walioshiriki mara nyingi fainali hizo.
Ukiacha kipa aliye kwenye kiwango bora, Benjamin Asare, pia uwepo wa Thomas Partey na Antoine Semenyo unakiongezea uimara mkubwa kikosi hicho.
Kocha ni Otto Addo, ambaye aliondoka baada ya Kombe la Dunia mwaka 2022. Amerejea kuchukua nafasi ya Chris Hughton aliyefukuzwa baada ya kuishia hatua ya makundi katika michuano ya AFCON ya mwaka 2024.
Ghana, kwa mujibu wa historia, watashiriki fainali zijazo wakiwa na ndoto za kuvuka robo fainali, hatua kubwa zaidi kwao katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Je, wataungana na Morocco ambayo kwa sasa ndiyo timu pekee ya Afrika kuwahi kuvuka robo fainali ya Kombe la Dunia? Morocco ilifika nusu fainali katika michuano hiyo mwaka 2022.

Related articles

Recent articles