CAIRO, Misri
VIGOGO wa soka la Afrika Magharibi, Ivory Coast na Senegal, zimekata tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia za mwakani.
Senegal ‘Simba wa Teranga’ wamefuzu baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mauritania, hivyo kujihakikishia nafasi ya kwanza katika Kundi B, wakiizidi pointi mbili DRC inayoshika nafasi ya pili.
Kwa upande wao, Ivory Coast wamefuzu kwa ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ katika mchezo uliochezwa mjini Abidjan.
Kwa matokeo hayo, mabingwa hao watetezi wa fainali za Mataifa Afrika (AFCON) wamefuzu Kombe la Dunia wakiwa kileleni wa Kundi, wakiizidi pointi moja Gabon inayoshika nafasi ya pili.
Ivory Coast waliocheza mechi zote 10 za kufuzu bila kuruhusu bao, wanarejea Kombe la Dunia wakiwa na kiu ya kuikosa michuano hiyo tangu waliposhiriki mwaka 2014.
Ni kwa maana hiyo basi, Ivory Coast na Senegal zinaunga na Morocco, Tunisia, Misri, Algeria, Ghana, Cape Verde na Afrika Kusini, ambazo nazo zimeshafuzu.
Published:


