EDINBURGH, Scotland
HUENDA mabosi wa Rangers ya Scotland wakamrejesha kwenye benchi la ufundi kocha wao wa zamani, Steven Gerrard.
Mkongwe huyo wa Liverpool mwenye umri wa miaka 45, amekuwa nje ya kazi tangu alipoachana na Al-Ettifaq ya Saudi Arabia mwanzoni mwa mwaka huu.
Siku chache zilizopita, Rangers walimfuta kazi Russell Martin, ambaye alisitishiwa ajira akiwa ameliongoza benchi kwa siku 123 pekee.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kile kilichoelezwa na Gazeti la Guardian, Gerrard hawezi kuvutiwa na mpango wa kurudi klabuni hapo.
Kiungo wa zamani huyo wa Liverpool na timu ya taifa ya England, aliondoka Rangers miaka minne iliyopita na kutimkia Aston Villa ya Ligi Kuu ya England.
Gerrard ana kumbukumbu nzuri alipokuwa kocha wa Rangers, ambapo aliiongoza timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu ya Scotland msimu wa 2020-21.
Mashabiki wa Rangers watakumbuka kuwa huo ulikuwa ubingwa wao wa kwanza wa Ligi Kuu tangu mwaka 2011.
Published:


