Munich, Ujerumani
MARA ya mwisho kwa mchezaji wa Ujerumani kutwaa tuzo ya Ballon d’Or ni miaka takribani 30 iliyopita. Ni Matthias Sammer aliyeibeba mwaka 1996.
Sammer alifanikiwa kuwa Mchezaji Bora wa tuzo hiyo baada ya kuipa Ujerumani taji la fainali za Mataifa ya Ulaya (EURO) na pia kuiongoza Borussia Dortmund kuwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kabla ya Sammer, Ujerumani iliwahi kubeba Ballon d’Or katika miaka ya 1970 na 1980 kupitia kwa Gerd Muller, Franz Beckenbauer na Karl-Heinz Rummenigge.
Hata hivyo, kwa miaka ya hivi karibuni, licha ya mafanikio ya timu ya taifa ya Ujerumani na klabu ya Bayern Munich, bado tuzo ya Ballon d’Or imebaki kuwa ndoto kwa mastaa wake.
Inaweza kuwaumiza mashabiki wa soka nchini Ujerumani kuona Thomas Muller, Toni Kroos, Oliver Kahn na Manuel Neuer, licha ya uwezo wao mkubwa na mafanikio waliyokuwa nayo, hawakuweza kuitwaa tuzo hiyo.
Lakini, kama ilivyo kwa wanasoka wengi duniani kote, uwepo wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ulikuwa kizingiti kikubwa kwao kwenye kinyang’anyiro cha Ballon d’Or.
Historia inaonesha kuwa kabla ya kiungo Luka Modric kuvunja utawala wao mwaka 2018, wawili hao walikuwa wameshinda tuzo hiyo kwa miaka 10 mfululizo.
Kwa upande mwingine, baada ya Ronaldo na Messi kuondoka barani Ulaya, sasa wanasoka wa mataifa mengine, ikiwamo Ujerumani, walau wana nafasi ya kutawala. Ni miaka mitatu sasa, wawili hao hawajaingia ‘top three’ ya tuzo hiyo.
Hivyo basi, Jamal Musiala wa Bayern Munich na Florian Wirtz (Liverpool) ni baadhi ya wachezaji wanaofanya vizuri katika soka la Ulaya, ambao kwa umri wao wa miaka 22, huenda wakaifuta machozi Ujerumani kwa kuibeba Ballon d’Or.
Published:


