13.4 C
New York

Utajiri uliojificha matamasha ya Simba, Yanga

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
HIVI karibuni, klabu kongwe za soka hapa nchini, Simba na Yanga, zilikuwa ‘bize’ kwa shamrashamra za matamasha yake ya ufunguzi wa msimu mpya wa 2025-26.
Simba, muasisi wa utamaduni wa matamasha hayo hapa nchini, ilitangulia, kabla ya wapinzani wao, Yanga, kufuata wikiendi iliyopita.
Kama ilivyo kawaida, Simba walicheza mchezo wa kirafiki, safari hii wakiwaalika majirani zao wa Kenya, Gor Mahia, wakati Yanga wao walicheza na Bandari FC, ambayo pia inatokea huko.
Kwa upande mwingine, ishu kubwa haikuwa matokeo ya mechi hizo. Na badala yake, tunaweza kujadili kwa kiasi juu ya uzito wa aina ya wapinzani walioletwa na klabu hizo za Kariakoo.
Ukiniuliza, nitakwambia kwamba kwa ukubwa wa Simba na Yanga kwa sasa, nikizingumzia Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hazikuhitaji kuzialika Gor Mahia na Bandari katika matamasha yao.
Siyo kwa maana ya kuzibeza Gor Mahia na Bandari, bali kwa kuangalia tofauti kubwa iliyopo sasa kati ya Simba na Yanga na klabu hizo za Ligi Kuu ya Kenya.
Kwa maana ya kulinda ‘brand’ na kuyaongezea thamani matamasha hayo na hata kuyafanya yakue zaidi, nafikiri Simba na Yanga zilihitaji kualika klabu za madaraja ya juu zaidi.
Najaribu kutolea mfano mataifa ya Afrika Kusini, Misri, Morocco au Tunisia, ambako klabu zao zina ufuasi mkubwa unaoweza kuinua kwa kiasi fulani ‘brand’ ya matamasha ya Simba na Yanga.
Hata kwa mtazamo wa kawaida tu, tunaweza kukubaliana kuwa mechi itakayozikutanisha Simba na Yanga dhidi ya wapinzani wa huko itakuwa na idadi kubwa ya mashabiki, ukilinganisha na zinapokutana na timu yoyote kutoka Ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Si tu kuongeza thamani ya matamasha, bali pia kuzialika klabu kama Al Ahly, Wydad Casablanca au Esperance de Tunis kunaweza kuwapa ladha halisi ya uwanjani mashabiki wanaolipa viingilio kutazama mechi.
Kwa upande mwingine, ni rahisi mno kuona mapato ya mechi dhidi ya timu hizo yakiwa makubwa, tofauti na Simba na Yanga zinapoamua kucheza na Gor Mahia na Bandari FC.
Wakati huo huo, bado nashawishika kujiuliza; kwanini bado viongozi wa Simba na Yanga hawajaona umuhimu wa kukaa mezani na kuona wanavyoweza kunufaika na utajiri wa mapato ya ‘derby’ katika matamasha yao?
Sijajua sababu ya msingi inayozuia Simba kuialika Yanga kwa ajili ya mchezo wa kirafiki katika Tamasha lake la ‘Simba Day? Sijui kwanini Yanga nao hawaoni tija ya kufanya hivyo.
Mwisho wa siku, ni kubishana na utajiri mkubwa wanaoweza kuvuna kuelekea msimu mpya. Pia, ni kuwapishanisha mashabiki na ladha nzuri ya derby ya mapema kuelekea msimu husika.
Mbali ya hapo, pia ni kulinda na kukuza ‘brand’ ya matamasha yao, wakati mwingine kuliko kuzialika Gor Mahia na Bandari FC, ambazo hata hivyo sibezi ushindani uliooneshwa na timu hizo katika mechi mbili tulizoshuhudia hivi karibuni.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img