LONDON, Uingereza
ULIMWENGU wa michezo umetikiswa na kifo cha lejendari wa ngumi za uzito wa ‘light welter’ nchini Uingereza, Ricky Hatton.
Kwa mujibu wa polisi wa jijini Manchester, walipigiwa simu na mtu asiyejulikana asubuhi ya Jumapili iliyopita na waliokwenda nyumbani kwa Hatton walikuta ameshafariki.
Siku mbili tu kabla ya taarifa za kifo chake, aliposti picha mitandaoni zikimuonesha akiwa ‘gym’ kujiandaa na pambano lake la hisani lililotarajiwa kupigwa Desemba 2, mwaka huu, mjini Dubai, Falme za Kiarabu.
Hatton aliyestaafu masumbwi mwaka 2012, ameondoka katika uso wa dunia akiwa na umri wa miaka 46. “Hakuna mshukiwa wa moja kwa moja kwa sasa,” ilieleza taarifa ya polisi.
Hadi anatangaza rasmi kuachana na mchezo wa ndondi miaka 13 iliyopita, bondia huyo alikuwa na rekodi ya kupigwa mara tatu pekee katika mapambano yake 48, akishinda 45, huku 32 akiwatwanga wapinzani kwa ‘KO’.
Hata hivyo, kabla ya mafanikio hayo, jina lake lilianza kupata umaarufu mkubwa mwaka 2005. Akiwa hana jina kubwa, aliwashangaza wengi baada ya kumdunda bingwa wa IBF, Kostya Tszyu.
ALIKUWA NOMA TANGU MDOGO
Thomas McDonagh ni bondia wa zamani, ambaye kwa sasa ni kocha. Alianza kumuona na kumfahamu Hatton tangu akiwa mdogo.
“Tangu akiwa na miaka 12, 13 na 14, alikuwa akishinda kwa KO dhidi ya watoto wenzake. Nilianza kumuona akiwa na miaka 10 au 11, wakati huo tayari alikuwa bondia mzuri,” alisema McDonagh.
VITA ZAKE NA MAYWEATHER, PACQUIAO
Mwaka 2007, akiwa ameshinda mapambano yote 43, Hatton alipoteza kwa mara ya kwanza alipodundwa na Floyd Mayweather mjini Las Vegas.
Kama itakumbukwa, maelfu ya mashabiki wake, akiwamo staa wa soka, David Beckham, walifunga safari kutoka Uingereza hadi Marekani kushuhudia pambano hilo.
Miaka miwili baadaye, alipoteza pambano lake la pili alipodundwa na mkali mwingine wa masumbwi, Manny Pacquiao.
ALITAKA KUJIUA
Mwaka 2011, baada ya kupoteza mbele ya Mayweather na Pacquiao, Hatton alijiona ameshakwisha. Anakiri kuwa alipitia wakati mgumu kutokana na msongo wa mawazo. “Wakati mwingine, niliweza kurudi nyumbani nikilia na kumwambia mpenzi wangu kuwa sitaki tena kuendelea kuishi,” alisema.
“Nilijiona nineshamaliza kwa upande wa ndondi. Niliona safari yangu imeishia hapo. Nakumbuka, nilijikuta nimegombana na wazazi, kocha wangu Billy Graham. Hali ilikuwa mbaya sana,” alisema.
Ni baada ya kurejea ulingoni, akapoteza pambano la tatu, alipopigwa na Vyacheslav Senchenko kwa KO ya raundi ya tisa mwaka 2012.
Alipopoteza pambano hilo, aliweka wazi kuwa hajioni akiwa na morali ya kuendelea na ngumi. “Sitaki tena kusita katika uamuzi wa kustaafu. Nimesikitika, siwezi kuendelea,” alisema.
STORI YAKE NA AMIR KHAN
Bondia aliyewahi kuwa bingwa wa dunia, Amir Khan, katika mahojiano yake na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alifichua namna Hutton alivyohusika katika mafanikio yake.
Khan, raia wa Uingereza kama ilivyo kwa Hatton, anakiri kuwa ushauri aliopewa na Hatton ulimsaidia kupata ushindi alipokwenda kupigana kwa mara ya kwanza katika ardhi ya Marekani.
Ni pambano lake dhidi ya Paulie Malignaggi. Khan alisema: “Aliniambia kuwa Paulie anatokea New York na sifa ya watu wa eneo hilo ni kuongea sana. Akaniambia natakiwa kuvumilia maneno yao ili yasinitoe mchezoni. Ndicho nilichofanya.”
Anaeleza pia, alikuwa akienda kujifua kwenye kambi ya Hatton. “Niliona alivyokuwa akijitoa. Ilinifanya niongeze jitihada,” alisema Khan, aliongeza kuwa bondia huyo alikuwa rafiki yake mkubwa nje ya ulingo.
AIKOSA ‘DERBY’ YA MANCHESTER
Hatton ni shabiki mkubwa wa Manchester City na huenda angekuwa jukwaani kuishuhudia timu hiyo ikiumana na Manchester United wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Etihad.
Kabla ya mchezo huo uliomalizika kwa Man City kushinda mabao 3-0, kulikuwa na ukimya wa dakika moja, pia wachezaji wa timu zote mbili wakivaa vitambaa vya rangi nyeusi ili kuomboleza kifo chake.
Kwa upande wake mashabiki, nao walifika nje ya nyumba yake jijini Manchester na kuacha maua, glovu za ngumi, jezi za Man City, achilia mbali kadi zenye meseji mbalimbali za kuomboleza kifo cha lejendari wao.
MASTAA WAMGUSIA KILA KONA
Miongoni mwa waliojitokeza kueleza kusikitishwa kwao na kifo cha Hatton ni mpachikaji mabao wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney.
Rooney alikuwa rafiki mkubwa wa Hatton. “Inasikitisha sana. Mkongwe, shujaa na mtu mzuri sana. Tupo pamoja na familia ya Rick,” aliandika Rooney katika akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Mkongwe mwingine wa Old Trafford, Roy Keane, ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa mechi za Ligi Kuu ya England, alisema: “Alikuwa shujaa, alijitoa kwa kila kitu kwa ajili ya ngumi.”
Kocha wa Man City, Pep Guardiola, hakupitwa na taarifa hizo mbaya za kifo cha Hatton. Kuelekea mchezo wao dhidi ya Man United, Mhispania huyo alisema:
“Kwa familia ya Man City, imekuwa ni siku mbaya. Ni kweli alikuwa bingwa wa dunia na shabiki wa Man City lakini kubwa zaidi ni kwamba familia imepoteza zaidi, alikuwa baba na babu pia.
Beki wa zamani wa Man City, Micah Richards, naye alimzungumzia Hatton akimtaja kuwa ni mtu wa watu. “Habari mbaya sana hii ya kifo chake. Si tu alikuwa shabiki wa Manchester City, bali pia alikuwa mtu wa watu,” alisema.
Published:


