13.1 C
New York

Nini chanzo ajali za ndege Afrika?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
MIEZI ya hivi karibuni imeshuhudia ajali za ndege zikitisa na kuacha majonzi barani Afrika, ikitosha kutolewa mfano katika mataifa ya Ghana na Kenya.
Agosti 6, helikopta ya kijeshi aina ya Harbin Z-9EH ya Ghana ilianguka Kusini mwa Mji wa Ashanti na kuua abiria wote nane, wakiwamo Waziri wa Ulinzi, Edward Omane Boamah, na Waziri wa Mazingira na Sayansi, Ibrahim Murtala Muhammed.
Siku moja tu baadaye, ndege ya madaktari nchini Kenya ilianguka katika makazi ya watu mjini Nairobi. Ni ajali iliyogharimu maisha ya watu sita.
Kabla ya ajali hizo, Sudan ilitikiswa na ajali ya ndege aina ya Beechcraft 1900D ilivyokuwa imebeba wafanyakazi wa kampuni ya mafuta. Ndege hiyo iliyoanguka muda mfupi tu baada ya kuanza safari, iliua watu 21.
Juni, mwaka jana, ndege aina ya Dornier 228 ilipata ajali nchini Malawi na kusababisha kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais, Saulos Chilima. Ni ajali iliyogharimu maisha ya watu tisa.
Kutokana na wingi huo wa ajali, maswali yamekuwa mengi juu ya ufanisi wa sekta ya usafiri wa anga barani Afrika. Nini chanzo cha ajali hizo?
Mosi, wataalamu wa sekta ya usafiri wa anga wanaamini makosa ya binadamu ndiyo chanzo kikubwa cha ajali hizo.
“Ndege hazina tatizo. Zimetengenezwa kwa ajili ya kuhudumia. Ndege zina vifaa maalumu, ambayo hata kabla ya tatizo kutokea, vitakuwa vimetoa taarifa kwa rubani au mhandisi,” anasema Godwin Ike, ambaye ni mshauri wa masuala ya usafiri wa anga nchini Nigeria.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo kupitia mahojiano yake na DW, ajali ni matokeo ya binadamu (rubani au mhandisi) kupuuzia ujumbe wa hatari anaopokea kutoka kwa vifaa maalumu vilivyomo kwenye ndege.
“Sasa, utakuta binadamu anakataa kushusha ndege hata pale mfumo unapobaini kuwapo kwa tatizo,” anasema Ike na kusisitiza kuwa bado kumekuwapo na tabia ya kupuuzia matengenezo.
Pili, wataalamu wanataja hali ya hewa kuwa ni chanzo kingine cha ajali za ndege. “Kwa upande wa sekta ya usafiri wa anga, hali ya hewa ni jambo la msingi mno. Baadhi ya maeneo yanapata mvua nyingi kuliko mengine, hivyo kuathiri hata uwezo wa (rubani) kuona vizuri,” anasema Felicity Ahafianyo, mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa nchini Ghana.
Hata hivyo, Ahafianyo anafichua kuwa bado kumekuwapo na upuuzaji wa taarifa za hali ya hewa katika mashirika ya ndege. “Niliwahi kuwa mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa katika ndege. Baadhi ya marubani hawajali kabisa kuhusu hali ya hewa,” anasema.
Akieleza zaidi, anasema rubani anapokumbana na changamoto ya hali ya hewa, taratibu zinamtaka kuomba kushusha ndege katika uwanja ulio karibu naye.
“Inasikitisha kuona marubani huwa hawafuati huu utaratibu, hasa wanapokuwa na viongozi wa Serikali, ambao muda wao huonekana mali zaidi kuupoteza kwa kushusha ndege kwa dharura,” anasisitiza Ike.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img