14.7 C
New York

Mtifuano kati ya Serikali na upinzani Ivory Coast, Uganda, Chad

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
KWA wiki chache za hivi karibuni, medani ya siasa barani Afrika imeshuhudia purukushani wanazopitia wanasiasa wa upinzani katika mataifa ya Ivory Coast, Uganda na Chad.
Kuanzia kuzuiwa kushiriki chaguzi, kunyimwa dhamana katika kesi zinazowakabili, hadi kuhukumiwa kifungo cha gerezani. Makala haya yanachambua zaidi.
IVORY COAST
Maandamano yanayoendelea nchini Ivory Coast ni matokeo ya kitendo cha kiongozi wa upinzani kuondoshwa katika kinyang’anyiro cha urais.
Maelfu ya raia wameingia mitaani mjini Abidjan ikiwa imebaki takribani miezi miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Ivory Coast, Taifa lenye watu milioni 32, ndilo lililo na uchumi imara zaidi kati ya yale yanayozungumza lugha ya Kifaransa kwa Ukanda wa Magharibi mwa Afrika.
Mwanzoni mwa mwaka huu, viongozi wanne wa upinzani, akiwamo Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, na Tidjane Thiam, walitangaza nia ya kugombea kugombea lakini Tume ya Uchaguzi imewazuia kushiriki Uchaguzi huo.
Thiam, ambaye ni Rais wa Chama cha Demokrasia cha Ivory Coast (PDCI), amezuiwa kushiriki Uchaguzi akiwa ndiye mpinzani mkubwa wa Rais wa sasa, Alassane Ouattara.
Ouattara, ambaye ana umri wa miaka 83, ameweka wazi kuwa atagombea, licha ya mihula yake mitatu ya kuliongoza Taifa hilo. Amedai kuwa nchi hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, ukiwamo mdororo wa hali ya usalama, hivyo inahitaji kiongozi mwenye uzoefu.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Ivory Coast, Thiam anakosa sifa kwa kuwa wakati anatangaza nia, alikuwa na uraia wa nchini mbili (Ivory Coast na Ufaransa).
Kwamba sheria za Ivory Coast zinazuia kwa namna yoyote mtu mwenye uraia-pacha kuwania nafasi nyeti ya urais.
Kwa upande wake, mwanaharakati Sagesse Divine, ambaye alishiriki maandamano, anasema ni suala lisilokubalika kwa Ouattara kuitaka awamu ya nne madarakani.
“Hatuitaki awamu ya nne na tunataka Tume ibadili uamuzi (wa kumrejesha Thiam), hicho ndicho tunachokitaka. Tunataka kuona wagombea wote wakipewa nafasi ya kushiriki Uchaguzi. Tunataka Uchaguzi wa haki,” anasema.
Kwa upande mwingine, siasa za Ivory Coast zimejijengea taswira ya chaguzi zenye presha kubwa na vurugu, kama ilivyotokea wakati Ouattara alipotangaza kuwania awamu ya tatu, ambapo mamia ya raia walipoteza maisha.
UGANDA
Hivi karibuni, Mahakama nchini humo ilimnyima dhamana kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, ambaye amekuwa rumande kwa takribani miezi tisa kutokana na tuhuma za uhaini.
Hayo yanakuja ikiwa imebaki miezi michache kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Januari, mwakani, ambao Rais Yoweri Museveni, licha ya umri wake wa miaka 80, ametangaza kugombea.
Besigye, ambaye ni mshirika wa zamani wa Rais Museveni, amepoteza mara zote nne alizowania kuingia Ikulu mbele ya mkongwe huyo.
CHAD
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mahakama nchini Chad ilimshushia hukumu ya kifungo cha miaka 20 gerezani aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wake, Succes Masra.
Mwanasiasa huyo anatajwa kuchochea mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Vurugu hizo za Mei, mwaka huu, zilitokea Kusini-Magharibi mwa Chad na kusababisha vifo vya watu 42, zikiwaathiri zaidi wanawake na watoto.
Hata hivyo, madai dhidi yake yamekuwa yakikosolewa na hata kuhusishwa na figisu za Serikali ya Rais Daby anayehofia kushindana na kiongozi huyo wa Chama cha Transformers.
Masra anafahamika kwa ushawishi wake mkubwa katika jamii ya Ngambaye inayopatikana Kusini mwa Chad, ambayo idadi kubwa ya watu wake ni waumini wa Ukiristo wanaoamini kuwa wamekuwa wakikandamizwa.
Msomi huyo wa masuala ya uchumi, alikuwa mwiba kwa Serikali ya Rais Daby, hadi pale alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, nafas aliyoitumikia kwa miezi mitano tu, kisha kujiuzulu.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, alimkabili Daby lakini alipoteza akiwa na asilimia 18.5 pekee ya kura, wakati mpinzani wake akikusanya asilimia 61.3.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img