Na Jonathan Benedict, Gazetini
Idadi inayoongezeka ya viongozi duniani sasa wanazingatia ujuzi wa kutumia Akili Unde au bandia (AI) kama sharti lisiloweza kupuuzwa wakati wa kuajiri wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Mwelekeo wa Kazi 2024 (Work Trends Index Annual Report), China inaongoza kwa asilimia 79 ya wafanyakazi wa maarifa (knowledge workers) wakisema hawatamuajiri mtu asiye na ujuzi wa AI. Vietnam inafuata kwa asilimia 76, ikibebwa karibu na India yenye asilimia 75.
Katika nafasi ya nne, Denmark na Indonesia zote zimepata asilimia 69, ishara kuwa mabadiliko ya kimataifa kuelekea umahiri wa AI yanaongezeka kwa kasi. Wastani wa nchi 31 uliyopimwa unasimama kwenye asilimia 66, huku Marekani ikiwa kidogo chini kwa asilimia 65.
Nchi nyingine zilizoonyesha viwango tofauti vya uelewa na matumizi ya AI ni Brazil na Ufaransa (zote asilimia 58), Uingereza (asilimia 57), huku Canada ikishika nafasi ya mwisho kwa asilimia 50.
Takwimu hizi zinaonyesha mabadiliko ya haraka katika soko la ajira, ambapo maarifa ya AI yanajitokeza kama faida kubwa ya ushindani kwa wafanyakazi hasa katika sekta zinazotegemea ujuzi wa kitaaluma na taarifa.
Je wewe una ujuzi upi kuhusu AI?


