11.6 C
New York

Kwanini viongozi Afrika hukimbilia kutibiwa nje?

Published:

LUSAKA, Zambia

HIVI karibuni, Afrika iliwapoteza marais wastaafu wawili kutoka mataifa ya Nigeria na Malawi, Muhammadu Buhari na Edgar Lungu, ambao wote walikuwa nje ya Bara hili kwa ajili ya matibabu.

Kufariki ni jambo moja lakini kwenda kutibiwa nje ya mataifa yao ni jambo linaloweka msingi wa makala haya.
Kwamba kwanini viongozi wa Afrika bado hawaziamini huduma za afya zinazotolewa na wataalamu wao wa ndani? Hoja iko hapo.

Kuziweka sawa takwimu, Waafrika zaidi ya 300,000, wakiwamo viongozi wa serikali, hufuata matibabu nchini India kila mwaka, safari hizo zikigharimu kiasi cha Dola za Marekani bilioni 2. Aidha, tatizo ni kubwa zaidi kwa Nigeria, takwimu zikionesha kuwa watu wake zaidi ya 5,000 hukimbilia nchini India kila mwezi. Safari hizo hugharimu Dola bilioni moja kwa mwaka.

Kutokana na biashara yake na wagonjwa kutoka Afrika, Serikali ya India huvuna zaidi ya Dola bilioni 6 kila mwaka, kiasi hicho kikitarajiwa kufikia wa Dola bilioni 13 mwaka 2026.

Akifungua mjadala huu, mtafiti wa masuala ya afya wa Nigeria, Jamila Atiku, anashangaa kuona viongozi, ambao kimsingi ndiyo wenye dhima ya kuboresha huduma za afya katika nchi zao, wakikimbilia ughaibuni kwa ajili ya matibabu.

Akitolea mfano nchini kwake, Nigeria, Jamila anasema: “Mfumo wa huduma za afya hapa Nigeria ni mbovu. Changamoto kubwa ni miundombinu. Hakuna dawa na pia kuna uhaba wa vifaa-tiba.”

Kwa upande wake, mwanaharakati wa haki za huduma za afya nchini Zimbabwe, Chamunorwa Mashoko, analiona tatizo hilo likiwa linaanzia katika uwekezaji mdogo katika sekta ya afya.

“Kati ya nchi 54 za Afrika, nyingi (32) hazina bajeti ya kutosha katika sekta ya afya. Haya ni matokeo ya kutegemea misaada kutoka nje,” anasema Mashoko katika mahojiano yake na DW.

Kuthibitisha hicho anachokisema msomi huyo, sekta ya afya kwa mataifa ya Afrika inategemea msaada wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 60 kutoka nje. Cha kusikitisha zaidi, viongozi wa Afrika wameonekana kupuuzia Azimio la Abuja la mwaka 2001, ambapo walikubaliana kuwa kila nchi itaelekeza asilimia 15 ya mapato yake ya bajeti katika sekta ya afya.

Kwa miaka zaidi ya 20 tangu Azimio hilo lilipopitishwa, ni nchi tatu pekee (Rwanda, Botswana na Cape Verde) zilizotekeleza. Katika hatua nyingine, Ripoti ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) inaeleza kuwa zaidi ya nchi 30 zenye uanachama wa Umoja wa Afrika (AU) huelekeza asilimia 10 tu ya bajeti kwenye sekta nyeti hiyo. Baadhi huelekeza asilimia 5 hadi 7 pekee.

Akizungumzia hilo, mtafiti wa Nigeria, Atiku, anasema sekta ya afya nchini Nigeria huendeshwa kwa asilimia 4 hadi asilimia 6 pekee. “Migomo ya madaktari na wataalamu wa afya haiwezi kuisha, wanalipwa mishahara midogo” anasema.

Katika kukabiliana na tatizo hilo kwa upande wa Nigeria, Serikali yake ina mpango ulioainishwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Iziaq Adekunle Salako.

“Bado tuna nafasi ya kuboresha sekta ya afya. Tunataka kufikia mwaka 2027 tuwe na uhakika wa vituo vya afya vya msingi visivyopungua 17,000,” anasema.

“Hakuna sekta ya afya iliyokamilika kwa asilimia 100. Naamini tupo katika njia sahihi ya kutafuta suluhisho.”
Kwa upande wake, Mashono anaitaka jamii kuacha kuwategemea wanasiasa, na badala yake kuzitumia rasilimali zake katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya inazozihudumia.

Wakati huo huo, Mashono anasema hata Azimio la Abuja la mwaka 2001, lililotaka serikali za Afrika kuwekeza asilimia 15 ya bajeti kwenye sekta ya afya, imepitwa na wakati.

“Asilimia 15 kwa sasa haitoshi na haiendani na uhalisia wa mazingira ya sasa. Ukilinganisha na wakati wa Azimio, yametokea mabadiliko mengi, ikiwamo ongezeko la idaadi ya watu na magonjwa,” anasema.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img