11.6 C
New York

Trump ameikabidhi Afrika mikononi mwa China?

Published:

PRETORIA, Afrika Kusini
MATAIFA ya Afrika yanakabiliwa na kiwango cha juu cha ushuru kwa bidhaa zake zitakazoingia Marekani, ikiwa ni sera ya utawala wa Rais Donald Trump.
Libya, Afrika Kusini, Algeria na Tunisia zimegongwa zaidi na sera hiyo, ambapo ongezeko la ushuru kwa mataifa hayo limefikia asilimia 25 hadi asilimia 30.
Aidha, mataifa mengine nane yamewekewa ushuru wa asilimia 15, kwa mujibu wa taarifa ya Alhamisi ya wiki iliyopita iliyotolewa na Ikulu ya Marekani.
Afrika Kusini, kwa upande wake, imelaani ushuru wa asilimia 30 iliyowekewa na Serikali ya Marekani, ikidai kuwa hatua hiyo haijatokana na sababu za kibiashara.
Kwa miaka michache ya hivi karibuni, Rais Donald Trump ameonekana kuwa na uhusiano mbaya na Afrika Kusini.
Matokeo ya uamuzi huo wa Rais Trump yameanza kuonekana, hasa katika Taifa dogo la Lesotho, ambalo limepandishiwa ushuru kwa asilimia 15.
Waziri Mkuu wa Lesotho, Samuel Matekane, amekiri kuwa ongezeko hilo la ushuru, pamoja na hatua ya Marekani kuiondoshea misaada, limeliathiri kwa kiasi kikubwa Taifa hilo lenye watu milioni mbili. Ni pamoja na viwanda kushindwa kujiendesha na kusababisha watu wengi kupoteza ajira.
Haijaishia huko tu. Hali ni mbaya pia kwa majirani zao, Afrika Kusini. Kabla ya tangazo la ushuru mpya, tayari kulikuwa na makontena ya matunda yaliyopaswa kupelekwa Marekani.
Sasa, kutokana na kupanda kwa ushuru, sehemu kubwa ya mzigo huo hautasafirishwa. Kwa ufupi, ni hasara ya mapema kabisa.
Wakati huo huo, sekta ya utengenezaji wa magari nchini Afrika Kusini nayo inatazamiwa ‘kupigika’ kutokana na ushuru mpya uliotangazwa na Serikali ya Trump.
“Tayari zipo kampuni (za kigeni) ndani ya sekta ya utengenezaji wa magari zimeanza kutishia kuondoka,” anasema Letswalo.
“Ushuru kuongezeka kutaibua mambo mengi. Mathalan, kama kampuni hizo zitaamua kuondoka Afrika Kusini, basi tatizo lililopo la uhaba wa ajira nalo litaongezeka mno.”
Lakini, kwa upande wa wataalamu wa uchumi, wanaamini hatua hiyo ni faida kwa China. Kwamba sasa wapinzani hao wa Marekani wanakwenda kuimarisha uhusiano wao kibiashara na mataifa ya Afrika.
“Sisi (Afrika) tunakwenda kujikabidhi moja kwa moja mikononi mwa China,” anasema Bismarck Rewane, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi nchini Nigeria.
Juni, mwaka huu, baada ya Rais Trump kusema atapandisha ushuru, kabla ya utekelezaji wake kuanza rasmi Agosti Mosi, Serikali ya China iliweka wazi mpango wake wa kuwapunguzia ushuru washirika wake wa kibiashara barani Afrika.
Naye mtafiti wa Afrika Kusini, Neo Letswlo, anaiona China kuwa ni fursa mpya kwa mataifa ya Afrika kukua zaidi kiuchumi. Akihojiwa na CNN, msomi huyo anazitaka nchi za Afrika kuikimbilia China kama mbadala wa Marekani.
“Marekani inaanza kupoteza hadhi yake ya kuwa kiongozi wa dunia. Nchi nyingi zinaanza kutokuitegemea Marekani na hii ni fursa kwa China,” anasema Letswalo.
Katika hilo la China kunufaika, Waziri wa Madini wa Afrika Kusini, Gwede Mantashe, ameeleza uwezekano wa Serikali yao kutafuta masoko mapya nje ya Marekani.
“Kama Marekani inaweka ushuru mkubwa, tunapaswa kutafuta masoko mengine. Kwa sasa, mshirika wetu namba moja katika biashara ni China, siyo Marekani. Marekani ni namba mbili,” anasema Mantashe.
Lakini, Letswalo anaiona hatari ya Afrika kuitegemea China kama mbadala wa Marekani katika biashara. Ni katika mazingira yapi?
Kwa mujibu wake, endapo Serikali za Afrika hazitavilinda viwanda vidogo katika ‘urafiki’ huo, basi vitauliwa na utitiri wa bidhaa za China. Anaonya kuwa Afrika inaweza kugeuzwa ‘dampo’ la bidhaa za China.
Anachokizungumzia msomi huyo kiliwahi pia kuibuliwa na Taasisi inayofuatilia uhusiano wa kibiashara kati ya China na mataifa yanayoendelea (CGSP).
Katika ripoti yake, CGSP haikuficha ukweli kwamba China imekuwa ikiweka mazingira ya kibiashara yanayowahumiza washirika wake.
Mathalan, China imekuwa ikiuza bidhaa ndondogo, ambazo nyingi zingeweza kuzalishwa na viwanda vya barani Afrika. Pia, bidhaa zake zinazokuja Afrika huwa zipo tayari kwa matumizi, tofauti na zinazokwenda kwao.
Mwaka jana, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, aligusia hilo la usawa wa kibiashara alipomtembelea mwenzake wa China, Xi Jinping, mjini Beijing.
Mwisho, Letswalo anaamini nje ya Marekani na China, ni wakati sahihi sasa kwa mataifa ya Afrika kuacha utegemezi na kuanza kuimarisha mtandao wa kibiashara miongoni mwao.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img