9.5 C
New York

Utafiti: Hewa chafu husababisha kupoteza kumbukumbu

Published:

LONDON, Uingereza

HEWA chafu ni moja ya sababu zinazoweza kuathiri uwezo wa ubongo wako kutunza kumbukumbu, kwa mujibu wa utafiti mpya wa Chuo Kikuu cha Cambridge cha Uingereza.

Kupoteza kumbukumbu ni ugonjwa unaotajwa kuwatesa watu takribani milioni 58 duniani kote. Kwa Uingereza pekee, ni watu 982,000, idadi hiyo ikitarajiwa kufikia milioni 1.4 mwaka 2040.

Kwa upande wake, utafiti wa Chuo Kikuu cha Cambridge ulilenga kubaini ni namna gani watu wanaoishi katika mazingira yenye hewa chafu walivyo hatarini kupata ugonjwa huo.

Katika utafiti huo ulihusisha watu milioni 29 duniani kote, wataalamu wa Cambridge walibaini kuwa hewa chafu aina ya PM25 inayopatikana katika moshi wa magari na viwandani unaweza kusababisha tatizo hilo.

Aidha, utafiti huo unaeleza kuwa hata kiwango kidogo tu cha hewa hiyo kinachangia ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu kwa asilimia 17.

Akizungumzia matokeo ya utafiti huo, Dkt. Haneen Khreis alisema jitihada zinahitajika katika kukabiliana na changamoto za hewa chafu.

“Kukabiliana na hewa chafu kuna faida kubwa katika masuala ya kiafya, kijamii na kiuchumi. Kutapunguza gharama za matibabu si tu kwa familia, bali hata kwa sekta ya afya,” anasema Dkt. Khreis.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Dkt. Mark Dallas, bado utafiti huo wa Cambridge umeacha maswali juu ya uhusiano kati ya hewa chafu na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu. “Bado tunapaswa kuelewa ni kwa namna gani hewa chafu inaingia na kuathiri ubongo,” anasema.

Utafiti wa Cambridge ni mwendelezo wa tafiti nyingi zilizowahi kueleza namna hewa chafu inavyoweza kuathiri ufanisi wa ubongo. Katika moja ya tafiti, ilielezwa kuwa mazingira yenye hewa chafu huweza kusababisha msongo wa mawazo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img