Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Halotel kupitia huduma ya HaloPesa ikishirikiana na timu ya Halotel Business Zanzibar, wamefanya mafunzo ya utafiti wa masoko na kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu matumizi ya teknolojia ya simu na huduma za kifedha.
Elimu hiyo imetolewa kwa wanafunzi hao Julai 8, 2025 visiwani Zanzibar baada ya timu ya kampuni hiyo kufanya ziara maalum katika chuo hicho.
Katika ziara hiyo, wanafunzi walipata fursa ya kujadili moja kwa moja kuhusu jinsi ambavyo huduma za HaloPesa zinaweza kuboreshwa zaidi ili ziendane na mahitaji halisi ya vijana wa kitanzania, hususan katika mazingira ya kielimu.

Kwa mujibu wa Ofisa Bidhaa na Masoko wa HaloPesa, Aidat Lwiza, katika mafunzo hayo walijadili zaidi umuhimu wa teknolojia ya simu katika kurahisisha maisha ya kila siku, hususan kupitia matumizi ya huduma ya fedha kwa njia ya simu ambayo inawawezesha vijana kufanya miamala kwa urahisi, haraka na kwa usalama zaidi.
“Tukiwa na lengo la kuimarisha upatikanaji wa mawasiliano bora na ya gharama nafuu kwa wanafunzi, tulifanikiwa pia kusajili laini za Halotel (EDU SIM), ambazo zinalenga kusaidia vijana kupata huduma za mawasiliano kwa vifurushi bomba na ubora wa hali ya juu,” amesema.

Aidha amesema kupitia mazungumzo na majadiliano hayo, waliweza kubadilishana mawazo na maoni juu ya namna bora ya kukuza huduma na kuhakikisha kwamba HaloPesa na Halotel inaendelea kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya vijana nchini.
Lwiza ameeleza kuwa kampuni imejipanga kuendelea kuwafikia vijana kwa karibu zaidi, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuwawezesha kupitia elimu ya teknolojia na huduma za kifedha.

“Tunaamini kuwa kwa kuwapatia vijana maarifa sahihi juu ya matumizi ya teknolojia na huduma kama HaloPesa, tunawawezesha si tu kufanya maamuzi bora, bali pia kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa kidijitali wa Tanzania,” amefafanua.


