19.8 C
New York

Rais Mwinyi: Tutamuenzi Charles Hilary kwa utendaji wake

Published:

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaongoza viongozi mbalimbali na mamia ya Wananchi katika maziko ya Marehemu Charles  Hilary, aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Ikulu.

Mapema, Rais Dk. Mwinyi aliwaongoza viongozi na Wananchi katika Ibada ya kuuaga mwili wa marehemu, iliyofanyika  viwanja vya Mapinduzi Square, Michenzani, Wilaya ya Mjini.

Akizungumza katika ibada hiyo, Rais Mwinyi amemuelezea Marehemu Charles Hilary kuwa ni mchapakazi, mcheshi, mtu wa watu, na mzalendo wa kweli aliyeipenda nchi yake kwa dhati.

Dk. Mwinyi amewaasa watendaji wa Serikali kuwa na utamaduni wa kuwasifu na kuthamini watendaji wazuri wakiwa hai, badala ya kusubiri mpaka wafariki dunia.

Aidha  amesisitiza kuwa Taifa lina wajibu wa kuendelea kumuenzi marehemu   kwa utendaji wake uliotukuka katika dhamana alizomkabidhi wakati wa uhai wake.

Vilevile,  ameifariji familia ya Marehemu Charles Hilary, akiwemo mjane wa marehemu, Sarah Mwakanjuki na kuwataka wawe na subira na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Misa ya kumuombea marehemu imefanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana, Mkunazini.
Akitoa salamu za familia, Mtoto wa marehemu, Faith Charles , ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa heshima kubwa aliyopewa baba yake wakati wa uhai wake, kwa kumuamini katika nyadhifa muhimu Serikalini na kumuaga kwa heshima baada ya kifo chake.

Marehemu  Charles  alifariki dunia Mei 11, 2025 akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Mlonganzila, Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu. Ameacha mjane na watoto wawili na mjukuu mmoja.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img