Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) limetangaza nafasi za kuandikishwa jeshini kwa vijana wa Kitanzania wenye elimu kuanzia Sekondari hadi elimu ya juu.
Tangazo hilo limetolewa leo April 30,2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano (JWTZ), Kanali Gaudentius Ilonda wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Kanali Ilonda amesema sifa za mwombaji ni lazima awe raia wa Tanzania mwenye kitambulisho cha Taifa,awe na afya nzuri na timamu,mwenye tabia na nidhamu nzuri,hajapatikana na hatia ya makosa ya jinai mahakamani na kufungwa, cheti halisi cha kuzaliwa, vyeti vya shule na taaluma.
Vilevile awe hajatumikia Jeshi la Polisi, Magereza,Chuo Cha Mafunzo au kikosi cha kuzuia Magendo,awe amehitimu Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT kwa mkataba wa kujitolea au mujibu wa sheria na kutunukiwa cheti.
Amesema kwa vijana wenye elimu ya kidato cha nne na kidato cha sita wawe na umri usiozidi miaka 24,Vijana wenye elimu ya Stashahada umri usiozidi miaka 26, vijana wenye elimu ya juu umri usiozidi miaka 27,na madaktari bingwa wa binadamu umri usiozidi miaka 35 ya kuzaliwa.
Sanjari na hayo utaratibu wa kutuma maombi kwa makundi yote mawili ni maombi yote yaandikwe kwa mkono na yawasilishwe Makao Makuu ya Jeshi Dodoma kuanzia Mei Mosi 2025 hadi Mei 14, 2025 yakiwa na nakala ya kitambulisho cha Taifa au nambari ya NIDA,akala ya Cheti Cha kuzaliwa,vyeti vya Shule na chuo, Nakala ya Cheti Cha JKT kwa waombaji waliomaliza mkataba wa kujitolea pamoja na nambari ya simu ya mkononi ya Mwombaji.
Hata hivyo ametoa angalizo kwa wananchi kutokubali kurubuniwa na matapeli kwa kudai hatua kali zitachukuliwa kwao ikiwemo kupelekwa Polisi.
“Naomba niwakumbushe hakuna nafasi ya kujiunga Jeshini kwa kutoa fedha atakae toa na kupokea Sheria ipo pale pale hatua Kali kwao zitachukuliwa,”amesema Kanali Ilonda.