15 C
New York

Majaliwa atoa maagizo sita kwa wadau wa kilimo

Published:

*Ahamasisha ushirika wa wakulima

Na Ramadhan Hassan, Gazetini-Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Aprili 27, 2025, ametoa maagizo sita kwa wadau wa sekta ya kilimo nchini, akisisitiza umuhimu wa wakulima kujiunga katika vyama vya ushirika vilivyosajiliwa ili kujiongezea nguvu ya kiuchumi na maendeleo ya pamoja.

Akizungumza katika Mdahalo wa Upatikanaji wa Fedha na Fursa za Maendeleo ya Ushirika sambamba na uzinduzi wa Ripoti ya Kilimo ya Mwaka 2023/2024 uliofanyika jijini Dodoma, Majaliwa amesema sekta ya kilimo ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa na inahitaji msukumo mpya kupitia ushirika imara na mifumo bora ya usimamizi.

Katika maagizo yake, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo kuimarisha utendaji wa wafanyakazi wake kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Agizo la pili, Majaliwa amezitaka taasisi za fedha kuendelea kushirikiana na vyama vya ushirika kwa kuweka mifumo rafiki inayowawezesha wakulima kupata huduma za kifedha kwa urahisi. “Hakikisheni mnapokutana nao, waambieni mambo yanayotekelezeka na yale yasiyotekelezeka ili waweze kujua na kupanga mikakati ipasavyo,” amesisitiza.

Katika agizo la tatu, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhakikisha upatikanaji wa teknolojia bora na pembejeo kwa wakulima ili kuwasaidia kufanikisha ndoto zao za maendeleo kupitia kilimo.

Agizo la nne ni kuhakikisha maandiko yote yanayohusu kilimo na ushirika yanaandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwafanya wakulima wengi zaidi kuelewa na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta hiyo.

Katika agizo la tano, Majaliwa amewataka wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali katika kujenga misingi imara ya ushirika, ili kizazi kijacho kipate mfumo thabiti wa kushiriki katika uchumi wa taifa kupitia sekta ya kilimo.

Agizo la sita lililolenga zaidi mawasiliano na taarifa, ni kuhakikisha ripoti za kila mwaka kuhusu kilimo zinatolewa kwa wakati ili wakulima wapate taarifa sahihi kuhusu hali ya lishe, upatikanaji wa chakula, pembejeo na mikakati ya kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Ushirika unaendelea Kuimarika

Waziri Mkuu Majaliwa amesema sekta ya ushirika nchini inaendelea kuimarika, hasa kwa wakulima wadogo, ambapo hadi sasa kuna zaidi ya vyama vya ushirika 7,000 vyenye wanachama zaidi ya milioni 8.

Ameeleza kuwa serikali ya Awamu ya Sita imefanya mageuzi makubwa ya sekta hiyo tangu mwaka 2017 kwa kusikiliza changamoto za wanaushirika, kutatua migogoro, kuboresha mifumo, kuimarisha masoko na huduma za kifedha, pamoja na kufungua ushirika kwa kuwaleta wanaushirika pamoja katika shughuli za kiuchumi.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha maendeleo ya ushirika kuwa ni pamoja na usimamizi usioridhisha, ukosefu wa uadilifu na dhamira thabiti kwa baadhi ya watendaji, pamoja na migogoro ya vyeo ndani ya vyama vya ushirika.

Programu ya BBT na mapendekezo ya sera ya ukopeshaji kwa Wakulima

Kuhusu utekelezaji wa Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT), Majaliwa amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikifanya jitihada za kutafuta rasilimali fedha ili kuimarisha utekelezaji wa programu hiyo yenye lengo la kuwawezesha vijana na wakulima wapya katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alitumia fursa hiyo kuomba kuwepo kwa sera maalumu ya ukopeshaji kwa wakulima ili kuondoa changamoto zinazowakabili katika upatikanaji wa mikopo na masoko.

“Kama nchi, lazima tuwe na sera maalumu ya ukopeshaji kwa sekta ya kilimo kwa sababu kilimo si sawa na biashara nyingine; kinahitaji uwekezaji wa muda mrefu,” alisema Bashe.

Bashe aliongeza kuwa ndani ya kipindi cha miaka miwili hadi mitatu ijayo, ushirika unatarajiwa kuwa na nguvu kubwa kiasi cha kuingia katika soko la hisa.

Akizungumzia kuhusu ripoti ya kilimo, Bashe alisema Watanzania wana haki ya kujua kinachoendelea kwenye sekta hiyo na hivyo taarifa zitakuwa wazi kwa umma ili kila mmoja aweze kusoma na kufuatilia maendeleo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img