25.8 C
New York

Infographic|Luis Diaz; alikataa Spurs, ametua Liverpool kwa Sh bilioni 85

Published:


Jembe la kazi lililotua Liver kwa bil. 85/-

KUELEKEA mwishoni mwa dirisha la usajili la Januari lililofungwa hivi karibuni, Liverpool walivunja kibubu na kutoa Pauni milioni 37 (zaidi ya Sh bil 85 za Tanzania) za kumsajili winga wa Porto, Luis Diaz.

Huku ada ya usajili hiyo ikitarajiwa kuongezeka na kufikia Pauni milioni 49, Diaz mwenye umri wa miaka 25 ameshasaini mkataba wa miaka mitano na nusu na kukabidhiwa jezi namba 23. Imeisha hiyo!

Kwa kuwa si wengi wanaoifuatilia Ligi Kuu ya Ureno, bila shaka jina la Diaz bado ni geni masikioni mwa mashabiki wa soka.

Ni nani huyo Diaz? Hilo ndilo swali. Katika makala fupi haya, hebu tiririka na mambo 10 yanayomuhusu winga huyo wa kimataifa wa Colombia.

  1. Tottenham waliamini anaelekea kwao baada ya kuweka mezani dau la Pauni milioni 46 lakini Diaz alikataa na kusema anataka kwenda kwa Jurgen Klopp.
  2. Wakati Argentina inanyakua taji la Copa America mwaka jana, Diaz aliyekuwa akiiongoza Colombia, alifungana na Lionel Messi katika ufungaji bora wa michuano hiyo. Kila mmoja alikuwa ameingia kambani mara nne.
  3. Msimu huu pekee, Diaz anayecheza winga ya kushoto akitumia mguu wa kulia, alishaifungia Porto mabao 16 na kutoa ‘asisti’ sita katika mechi 28 za mashindano yote.
  4. Kati ya mechi 18 za Ligi Kuu ya Ureno alizokuwa ameshuka dimani msimu huu, ni nne tu zilizomalizika akiwa hajafunga au kutoa pasi ya bao (asisti).
  5. Uwezo wake mkubwa wa kukokota mpira, pasi za uhakika na mashuti makali, vinamfanya afananishwe na staa wa England anayekipiga Manchester United, Jadon Sancho.
  6. Kwanini Klopp amemsajili? Mosi, huyu ndiye mrithi wa Mohamed Salah. Pili, amepelekwa Anfield ili akawape changamoto Salah, Sadio Mane na Diogo Jota.
  7. Chukua hii; Diaz aliyeondoka Porto akiwa ameitumikia tangu ilipomsajili mwaka 2019, anakuwa mchezaji wa kwanza raia wa Colombia kuichezea Liverpool.
  8. Alianza kuichezea timu ya taifa ya Colombia mwaka 2018 na tangu hapo hajawahi kuacha kuitwa. Mwaka jana, aliiwezesha kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Copa America.
  9. Kwa upande mwingine, ujio wake Liverpool unaibua hofu kwamba huenda Mane anajiandaa kuondoka. Mkataba wa Msenegal huyo umebakiza miezi 18.
  10. Kipa wa Liverpool raia wa Brazil, Alisson, ni shabiki mkubwa wa Diaz. “Luis Diaz ni bonge la mchezaji. Ni mzuri kwenye ulinzi na pia anafunga. Alionesha hilo kwenye Copa America,” alisema Alisson.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img