11.3 C
New York

Infographic| Unaipenda Yanga, unafahamu yanayokugusa Katiba Mpya?

Published:

MIEZI michache iliyopita, klabu ya Yanga katika Mkutano Mkuu wake iliwasilisha kwa wananchama wake mabadiliko 10 yatakayofanyika katika Katiba yake.

Ifahamike kuwa hiyo ni hatua ya vigogo hao wa soka la Tanzania kuelekea kwenye mabadiliko ya kiuendeshaji wa klabu.

Je, ikiwa ni miezi takribani minne imepita tangu Yanga ulipofanyika Mkutano Mkuu huo, haya ndiyo maeneo yatakayoguswa kwenye mabadiliko hayo ya Katiba.

Sifa ya mgombea

Kwa mujibu wa Katiba mpya, sifa za mgombea wa kiti cha urais katika klabu ya Yanga anapaswa kuwa na kiwango cha elimu kisichopungua ngazi ya Shahada ya Chuo Kikuu. Anayegombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji awe na walau elimu ya kidato cha nne.

Aidha, mgombea anapaswa kuwa mwanachama hai wa Yanga kwa kipindi kisichopungua miaka minne mfululizo, bila kusahau umri wa kuanzia miaka 25 na usiozidi miaka 75.

Idadi ya wajumbe Mkutano Mkuu

Awali, kila mwanachama alikuwa anaruhusiwa kuingia kwenye Mkutano Mkuu lakini Katiba Mpya itaruhusu wawakilishi watano pekee kutoka kila tawi.

Gharama za uanachama

Kwa sasa, gharama za kuwa mwanachama wa Yanga ni Sh. 15,000 (ada ya mwaka Sh 12,000, Kadi Sh 2,000 na fomu Sh 1,000). Hata hivyo, Katiba Mpya inatamka gharama za uanachama ni Sh 36,000 (ada ya mwaka ni Sh 24,000, Kadi Sh 10,000 na fomu Sh 1,000).

Wajumbe Kamati ya Utendaji

Pia, Ibara ya 28 ya Katiba ya sasa imefanyiwa mabadiliko na kushuhudia kupungua kwa idadi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji. Kwa sasa, ni 13 lakini Katiba Mpya itawapunguza na kubaki tisa (Rais, Makamu wake, Wajumbe watano wa kuchaguliwa na wajumbe wawili wa kuteuliwa na Rais).

Majukumu ya Rais

Kuna mabadiliko ya Ibara ya 33, ambapo klabu itakuwa inaongozwa na Rais na si Mwenyekiti kama ilivyo sasa. Vilevile, Makamu wake ameongezewa majukumu, ambapo Katiba Mpya itamtambua pia kama Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango.

Sekretarieti ya Yanga

Katiba Mpya itaitambua kwa jina la Timu ya Menejimenti na itakuwa na idara nne.

Mgawanyo wa Hisa

Badiliko hilo limeafanywa katika Ibara ya 56. Katika Katiba Mpya, Kampuni ya Umma ya Yanga itaitwa Kampuni Binafsi za Yanga. Katika mgawanyo wa hisa, asilimia 51 zitamilikiwa na klabu (wanachama), huku asilimia 49 ikiwa chini ya wawekezaji.

Juu ya asilimia 49 za wawekezaji, zitapaswa kugawanywa kwa watu tofauti wasiozidi wanne na wasiopungua watatu. Ikimaanisha, kila mmoja atamiliki si zaidi ya hisa asilimia 12.25.

Wakati huo huo, itakuwapo Bodi ya kuendesha Kampuni na wanachama watawakilishwa na wajumbe watano.

Adhabu kwa mwanachama

Katika badiliko la Ibara ya 55 litaitaka Kamati ya Utendaji kushirikisha vyombo vya haki na vya kimahakama vya klabu kabla ya kumfukuza mwanachama, tofauti na ilivyo sasa ambapo Kamati ina mamlaka ya kujichukulia uamuzi.

Mashabiki kutambuliwa

Ibara ya tano iliguswa na mabadiliko, tofauti na awali ambapo klabu ilitambua aina mbili tu za wanachama; wanachama kamili na wale wa heshima. Katiba Mpya itawatambua mashabiki kwa kuwa watapewa kadi za kijano, huku zile za njano zikimilikiwa na wanachama.

Idadi ya wanachama  

Katiba ya sasa kupitia Ibara ya 62, haijaweka ukomo wa idadi ya wanachama katika matawi, ingawa inataka wasipungue 100. Sasa, Katiba Mpya imeendelea kusisitiza idadi ya chini kutpungua 100, huku ukomo ukitakiwa kuwa wanachama 500.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img