1.6 C
New York

Visualization| Mwakinyo na rekodi, ubabe wake ulingoni

Published:

JINA la Hassan Mwakinyo limeendelea kuchukua nafasi yake kwenye mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini, hasa baada ya kumtwanga bondia wa kimataifa wa Namibia, Julius Indongo.

Pambano hilo la uzito wa super welter lilipigwa katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam na Mwakinyo akaibuka mbabe kwa KO ya raundi ya nne na kuutetea mkanda wake wa Shirikisho la Ngumi Afrika (ABU).

Apanda viwango duniani

Kabla ya pambano hilo, Mwakinyo mwenye uzito wa kilogramu 69, alikuwa anashika nafasi ya 24 kati ya mabondia 1,527 wa uzito wa Super welter duniani kote.

Baada ya kumtandika Mnamibia hivi karibuni, sasa amepanda kwenye chati hiyo na sasa ni wa 13 duniani, huku akishika namba moja Afrika.

Mkali wa KO

Dhidi ya Indongo lilikuwa pambano la 22 kwa Mwakinyo tangu aanze masumbwi ya kulipwa mwaka 2015.

Kati ya hayo 22, mwanamasumbwi huyo mwenye umri wa miaka 26 ameshinda 20 (14 kwa KO) na kupigwa mara mbili pekee.

Miaka 4 bila kupigwa

Ndiyo, ni miaka minne sasa imepita tangu Mwakinyo alipopoteza pambano dhidi ya Lendrush Akopian, ambalo Mwakinyo alipigwa kwa pointi jijini Moscow, Urusi.

Tangu kipindi hicho, ameshinda mapambano yote 10, matatu tu kati ya hao akifikisha wapinzani wake raundi ya mwisho (12).

Aidha, mara ya mwisho kuona Mwakinyo akipigwa kwa KO ilikuwa mwaka 2016, alipoingia kwenye ’18’ za Mtanzania mwenzake, Shabani Kaoneka.

Pia, katika mapambano yake 22, amekutana na mabondia wa kigeni mara tisa, huku akivaana na Watanzania wenzake mara 13.

Pambano lililompa kiki

Licha ya kuanza ngumi za kulipwa mwaka 2015, pambano lake la kwanza likiwa ni dhidi ya Alibaba Tarimo, jina la Mwakinyo lilikuwa maarufu zaidi mwaka 2018.

Hiyo ilikuwa ni baada ya kumdunda bondia raia wa Uingereza, Sam Eggington, tatika pambano lililopigwa katika Jiji la Birmingham nchini humo.

Huku likiwa ni pambano la utangulizi, siku ambayo staa wa ndondi duniani, Amri Khan, alikuwa akizichapa na Samuel Vargas, ilichukua dakika sita tu kwa Mwakinyo kummaliza Eggington kwa KO ya raundi ya nne.

Kwani yeye anasemaje?

“Kwanza, ningependa kumshukuru Mungu kwa baraka zake kwa sababu nilikuwa naisubiri kwa muda mrefu nafasi hii. Pia, ningependa kuishukuru familia yangu, hasa mama yangu, Fatuma Hassan, kwa kuniunga mkono.”

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img