10.9 C
New York

Neymar ana nafasi Kombe la Dunia 2026?

Published:

RIO, Brazil
WAKATI Ousmane Dembele anaitwaa tuzo ya mwaka huu ya Ballon d’Or, Neymar alikuwa kitandani akisikilizia maumivu ya upasuaji. Ni majeraha yake ya tatu ndani ya mwaka mmoja.
Majeraha yamekuwa sehemu ya maisha ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 tangu aliporejea katika klabu yake ya zamani ya Santos mwanzoni mwa mwaka huu.
Ni kutokana na mfululizo wa majeraha, sasa Neymar anabaki njiapanda juu ya uwezekano wa kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani.
Hivi karibuni, kocha wa timu ya taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti, alitangaza kikosi kitakachocheza mechi za kufuzu fainali hizo dhidi ya Korea Kusini na Japan lakini jina la Neymar halikuwamo.
Neymar hajacheza mechi yoyote chini ya Ancelotti na amekuwa nje ya kikosi cha Brazil kwa miaka miwili sasa. Mara yake ya mwisho kuwa kikosini ni katika mchezo wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uruguay mwishoni mwa mwaka 2023.
Kwa upande wake, beki wa zamani wa Brazil, Cafu, anaiona nafasi finyu kwa Neymar kuwa sehemu ya kikosi hicho kitakachoshiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika katika mataifa matatu ya Marekani, Mexico na Canada.
“Kwa miaka 15 iliyopita, Neymar alikuwa staa, alibeba matarajio makubwa ya kikosi. Lakini, huwezi kutwaa Kombe la Dunia ukiwa peke yako. Ni ngumu kumtegemea kwa sasa kwa sababu hawezi hata kucheza mechi tatu mfululizo (kutokana na majeraha),” anasema.
Hata hivyo, licha ya majeraha, bado Neymar, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Brazil (mabao 79), amekuwa na mchango mkubwa kikosini kila anapopata nafasi ya kucheza.
Hilo linathibitishwa na Taasisi ya utafiti ya Datafolha, ambayo inaeleza kuwa asilimia 48 ya mashabiki wa soka nchini Brazil bado wanataka kuona mshambuliaji huyo akijumuhishwa kikosini.
Miongoni mwa wanaoamini bado Brazil inanihitaji huduma ya Neymar ni mpachikaji mabao wa zamani wa timu hiyo, Ronaldo de Lima ‘Phenomenon’.
Ronaldo, baada ya kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu kama ilivyo kwa Neymar, alicheza kwa kiwango kikubwa na kuipa Brazil taji la Kombe la Dunia mwaka 2002.
“Ni mchezaji muhimu kwa Brazil. Kwa sasa, hatuna kama Neymar,” anasema Ronaldo katika mahojiano yake ya hivi karibuni mjini Sao Paulo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img