11.6 C
New York

Soka la Ujerumani na changamoto ya ubaguzi wa rangi

Published:

MUNICH, Ujerumani
LICHA ya jitihada kubwa za Chama cha Soka, klabu na baadhi ya mashabiki, bado imeonekana ni ngumu kuondosha vitendo vya ubaguzi dhidi ya wachezaji wenye ngozi nyeusi.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Ligi hivi karibuni, nyota wa Schalke 04, Christopher Antwi-Adjei, alikuwa gumzo nchini humo.
Ni baada ya tukio lake la kufanyiwa ubaguzi na mashabiki wa Lokomotiv Leipzig inayoshiriki Ligi Daraja la Nne ya Ujerumani.
Antwi-Adjei alichelewa kwa dakika kadhaa kurusha mpira baada ya kukerwa na kauli ya kibaguzi kutoka kwa shabiki aliyekuwa jukwaani.
Mshambuliaji huyo alimwambia maamuzi msaidizi, hali iliyosababisha mchezo huo kusimama kwa dakika kadhaa.
Hata baada ya mchezo kuendelea, bado Antwi-Adjei alikuwa kwenye wakati mgumu baada ya mashabiki wa Lokomotiv Leipzig kumzomea kila alipogusa mpira.
Haikuwa mara ya kwanza kushuhudia ‘uhuni’ huo katika soka la Ujerumani. Mwaka 2021, vitendo vya ubaguzi vilisababisha mwamuzi kumaliza mchezo kati ya Duisburg na Osnabruck.
Pia, mwaka 2023, mamlaka za soka nchini Ujerumani zilipokea jumla ya malalamiko ya 762 ya vitendo vya ubaguzi, nyinyi zikihusisha mechi za madaraja ya juu. Kati ya matukio hayo, 220 (29%) yalikuwa ya ubaguzi wa rangi.
Kama hiyo haitoshi, msimu wa 2023-24 ulimalizika kukiwa na mechi takribani 900 kumalizwa kabla ya muda kutokana na vitendo vya ubaguzi wa rangi. Ripoti za waamuzi zilionesha matukio 2,500 ya aina hiyo.
Akizungumzia kukithiri kwa matukio ya aina hiyo, Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, alisema:
“Tunachoweza kufanya ni kuzitoza faini klabu, kupunguza pointi na kuzitaka timu kucheza bila mashabiki,” alisema Infantino.
Kwa upande wake, Chama cha Soka cha Ujerumani (DFB) kimeeleza kusikitishwa na uwepo wa matukio ya ubaguzi wa rangi katika mechi zake.
“Ubaguzi hauna nafasi katika soka. Tunasimamia utu na heshima,” alisema Rais wa DFB, Bernd Neuendorf.
Je, ni hatua zipi anazopaswa kufuata mwamuzi endapo vitendo vya ubaguzi vinajitokeza wakati wa mchezo?
Kwa mujibu wa FIFA, zipo hatua tatu za kufuata. Mosi, ni kusimamisha mchezo kwa muda na kuwatangazia mashabiki sababu ya kufanya hivyo.
Pili, endapo wataendelea, mwamuzi atalazimika kuwarudisha vyumbani wachezaji ili kuona kama itasaidia kumaliza kelele (za ubaguzi) kutoka kwa mashabiki.
Tatu, endapo bado wataendelea, basi mwamuzi atamaliza mchezo moja kwa moja. Ni kama ilivyotokea mwaka 2021, mwamuzi alipomaliza mechi ya Daraja la Tatu kati ya Duisburg na Osnabruck.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img