LONDON, England
MSIMU ujao wa 2025-26 uko njiani, ukitarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi ujao. Ni Ligi Kuu ya England (EPL), michuano ya soka inayotajwa kufuatiliwa zaidi katika ulimwengu wa mchezo huo wa mpira wa miguu.
Huku Liverpool ikitwaa taji, Arsenal ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya pili kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo pia 2023-24.
Kuelekea msimu ujao, mchambuzi wa kandanda wa kituo cha runinga cha Sky Sport, Alex Keble, anajiuliza maswali sita (6) yanayosubiri majibu.
AMORIM WA MAN UNITED ‘ ATATOBOA’ ?
Kama kuna kocha mwenye presha kubwa ya kufanya vizuri kwa msimu ujao, basi ni huyu wa Manchester United, Ruben Amorim.
Msimu uliopita, alikusanya pointi 27 tu katika mechi 27 za EPL, idadi ndogo zaidi kuwahi kuwa nayo Man United katika historia ya Ligi Kuu hiyo.
Kama hiyo haitoshi, Amorim ana asilimia 38.1 ya ushindi wa mechi alizokaa kwenye benchi, wastani mdogo zaidi kuliko makocha wote waliopita Old Trafford tangu mwaka 1971 na 1972.
MAN CITY, CHELSEA KUPOTEZWA?
Fainali za Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu zilizomalizika hivi karibuni zinaweza kuziathiri klabu hizo.
Manchester City ilifika robo fainali, wakati Chelsea walitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuifunga PSG.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola, alikiri hilo akisema: “Huenda yakawa ni majanga kwa mechi zetu za Novemba, Desemba au Januari. Tumechoka na tumechoshwa na Kombe la Dunia.”
LIVERPOOL KUTETEA UBINGWA?
Msimu uliopita, kocha Arne Slot alinyakua ubingwa wa EPL akiwa hajasajili mchezaji mpya, akitumia kikosi alichoachiwa na mtangulizi wake, Jurgen Klopp.
Safari hii, baada ya kuwapoteza Trent Alexander-Arnold na Andy Robertson, Mholanzi huyo ameingia sokoni na kuwasajili walinzi wengine wa pembeni, Milos Kerkez na Jeremie Frimpong.
Wakati huo pia, Slot amevunja rekodi ya usajili klabuni hapo kwa kumchukua Florian Wirtz kutoka Bundesliga alikokuwa akiitumikia Bayern Leverkusen.
NI WAKATI WA NEWCASTLE UNITED?
Newcastle imekuwa tishio jipya kwa vigogo wa EPL tangu klabu hiyo iliponunuliwa na matajiri wa Saudi Arabia.
Kwa miaka mitatu ya hivi karibuni, Newcastle imeshiriki mara mbili kwenye michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa.
Ni wazi sasa kocha wake, Eddie Howe, ataekekeza nguvu kubwa katika vita ya kuliwania taji la EPL.
NINI HATIMA YA WOLVES, BRENTFORD?
Timu hizo zimewauza wachezaji wake tegemeo, kama zilivyo Bournemouth na Nottingham Forest.
Brentford iko hatarini zaidi kwani iliwapoteza Christian Norgaard na Bryan Mbeumo, achilia mbali kocha wao wa miaka saba mfululizo, Thomas Frank, aliyetimkia Tottenham.
ZUBIMENDI, GYOKERES KUIBEBA ARSENAL?
Katika eneo la ulinzi, kocha Mikel Arteta ameimarisha kikosi chake kwa kumsajili Martin Zubimendi kutoka Real Sociedad.
Zubimendi alifanya kazi nzuri akichukua nafasi ya Rodri katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania kilichotwaa ubingwa wa fainali za EURO zilizopita.
Pia, kupitia usajili wa majira haya ya kiangazi, Arteta ameboresha safu ya ushambuliaji kwa kumchukua mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ureno msimu uliopita, Viktor Gyokeres.
Je, wawili hao wataiwezesha Arsenal kumaliza ukame wa taji la EPL? Mara ya mwisho kwa Washika Bunduki kuibeba ‘ndoo’ hiyo ni msimu wa 2003-04.


