Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema anatamani kuona Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) inakuwa kimbilio la walimu ambao ni kundi kubwa katika utumishi wa umma kwa kutenda haki pindi inaposhughulikia mashauri ya nidhamu na rufaa za walimu
Amesema haifurahishi kuona walimu wanapoteza ajira kwa ukiukaji wa sheria, kanuni na karatibu katika utumishi wa umma ilihali TSC ipo.
Simbachawene ametoa kauli hiyo jana Juni 5,2025 wakati akifunga mafunzo ya Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Walimu yaliyofanyika kwa muda wa siku tatu katika Chuo Cha Utumishi wa Umma, Tanzania, Kampasi ya Tabora.

Amesema TSC ndiyo mlezi wa walimu, hivyo wajumbe na watumishi wa Tume hiyo watoe elimu kwa walimu katika masuala muhimu yanayohusu utumishi wao kwa kuzingatia jukumu lake la ulezi, adhabu ya kufukuzwa kazi iwe ni hatua ya mwisho pale inapotokea mwalimu kutotii yale anayoelekezwa.
Kufuatia hatua hiyo, Simbachawene amewataka Maofisa Elimu walioteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati za Ajira, Upandishaji Vyeo na Nidhamu wa Tume ya Utumishi wa Walimu ngazi ya Wilaya wakatumie mafunzo hayo waliyoyapata kama nyenzo ya kuboresha utendaji kazi kwa kutoa haki kwa walimu wenye mashauri ya nidhamu na rufaa.

” Ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya hatutasikia au kuona uamuzi wa shauri unakatiwa rufaa Tume ya Utumishi wa Walimu Makao Makuu kwa kuamuliwa bila kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni na taratibu zinazowaongoza katika kufikia uamuzi kwa haki na usawa” amesema.
Ametoa rai kwa wajumbe hao kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa mashauri ya nidhamu pindi wanaposhughulikia mashauri ya nidhamu na rufaa.
Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu Prof. Masoudi Muruke amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha kunakuwa na walimu ambao wanajituma na wanaozingatia maadili ya kazi yao kwa ajili ya kuwalea watoto kwa usahihi na hivyo kuboresha elimu nchini kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.


